Dube, Ciaoba wabeba tuzo

Muktasari:

Katika mechi 45 za Ligi Kuu Bara zilizochezwa mpaka sasa yamefungwa jumla ya mabao 74, huku Simba ikiongoza kwa kufunga mabao 14, ikifutiwa na Azam yenye tisa katika mechi tano kwa kila moja.

STRAIKA wa Azam na kinara wa mabao kwa sasa katika Ligi9 Kuu Bara, Prince Dube ametangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ndani ya Septemba, huku Kocha Mkuu wake, Aristika Cioaba akishinda tuzo ya Kocha Bora wa mwezi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi (TPLB), Dube aliyesajiliwa msimu huu kutoka Highlander ya Zimbabwe amenyakua tuzo hiyo kwa kufanya vyema ndani ya Septemba kwa kuifungia timu yake mabao matatu katika mechi nne alizoichezea ndani ya mwezi huo.

Ciaoba aliiongoza Azam kushinda mechi nne mfululizo ndani ya Septemba mara baada ya ligi kuanza Sept 6, huku Dube akifunga mabao matatu.

Tayari ndani ya Oktoba kocha huyo na straika wake wameshaanza mambo kwa kushinda mechi moja dhidi ya Kagera Sugar kwa kuinyoa mabao 4-2, huku Dube akifunga mawili na kumfanya awe kileleni kwa orodha ya wafungaji akimzidi bao moja Mfungaji Bora wa misimu miwili iliyopita, Meddie Kagere wa Simba mwenye mabao manne.