Donjo Janja awalipua wanaomfuatilia

Friday October 5 2018

 

By Nasra Abdallah

SIKU moja baada ya msanii Dogo Janja kuonekana akiwa na mwanasaikolojia maarufu, Chris Mauki, ameamua kufunguka sababu za kukutana naye.

Kuonekana kwake huko kulitafsiriwa huenda alienda kupata ushauri wa kisaikolojia baada ya kuwepo kwa tetesi amebwagawa na mrembo, Irene Uwoya ambaye ni mke wake.

Akilizungumzia hilo, Dogo Janja alisema hakuna kitu kama hicho kwani alienda huko kwa ajili ya masuala yake ya biashara.

Hata hivyo, alipoulizwa Mauki ni mtu wa aina gani, alisema ni mtu mwema na kimbilio la watu wenye matatizo na aliwahamasisha wengine wanaokabilia na tatizo la kisaikolojia kutosita kwenda kwake.

Kuhusu sakata la mke wake Uwoya, kama habari zilizopo ni kweli amebwagwa, Dogo anayetokea pande za Arusha, alisema hazina ukweli wowote kwani hayo ni maneno ya watu.

“Hivi mtu una ushahidi gani kama mimi na mke wangu tumebwagana, hakuna kitu kama hicho na mtasubiri sana.

“Hayo mnayoyaona anayoyafanya Uwoya akiwa mbali na mimi eleweni kuwa nina taarifa nayo yote na isitoshe sisi sio watu wa kufuatanafuatana kwani kila mtu ana shughuli zake za kumwingizia kipato,” alisema Dogo anayetesa na wimbo wa Banana kwa sasa.

Kwa takriban mwezi sasa, Uwoya ameonekana akiwa anakula bata maeneo mbalimbali huku akiwa katika mavazi ya kila aina ya gharama na amekuwa akionekana peke yake bila ya Dogo na wakati mwingine akionekana na wanaume tofauti, hali inayozidi kuzua maswali.

Kama vile haitoshi, hivi karibuni alipokuwa akiumwa na kulazwa hospitali, mrembo huyo kama mke halali wa Dogo hakuonekana hospitali, wala kumpa pole katika ukurasa wake wa Instagram ambao amekuwa akitupia mambo mbalimbali jambo lililozidi kuzua maswali.

 

 

 

Advertisement