Dk Msolla kumbuka dawa ya deni kulipa hakuna namna

Tuesday August 13 2019

 

By Andrew Kingamkono

Ukitaka ubaya dai chako… ndicho kinachowakuta nyota watatu wa Yanga, Kelvin Yondani, Juma Abdul na Andrew Vincent ‘Dante’.

Wachezaji hawa watatu wamegoma kufanya mazoezi na timu hiyo wakishindikiza kulipwa mishahara yao pamoja na fedha zao za usajili walizoahidiwa msimu uliopita.

Wachezaji hao wameshangazwa na kitendo cha viongozi wao kusajili wachezaji wapya kwa madau makubwa, lakini wameshindwa kulipa stahiki zao.

Wakati wakifanya mgomo huo Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla amesema suala la wachezaji hao kugoma si haki kwasababu wapo wachezaji wengine wengi wanaodai, lakini hawajagoma.

Huku akisema suala lao amelipeleka kwa Kocha Mwinyi Zahera ndiye atakayeamua kwamba anawataka kambini au la.

Nadhani Dk Msolla amesahau ule usemi unaosema dawa ya deni kulipa wala siyo vitisho anavyotaka kuwaletea wachezaji hao.

Advertisement

Nadhani Dokta amesahau kwamba ukiwa na njaa ni vigumu kujituma uwanjani, ukiangalia jitihada kubwa aliyofanya kutafuta fedha alipaswa kumaliza kwa kulipa wachezaji hao waliopambana katika mazingira magumu msimu uliopita.

Hakuna anayebisha kwamba Yanga ni kubwa kuliko mtu yeyote, ila ni wajibu wa kiongozi kuhakikisha wachezaji wake wanapata mishahara na posho zao kwa wakati ili kuwaongezea moyo wa kujituma.

Hata hao wachezaji wapya wasipokuwa na uhakikia wa mishahara hawataweza kujituma uwanjani hivyo ile ndoto ya Yanga kutwaa ubingwa msimu huu pamoja na kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa haitafanikiwa hata kidogo.

Hatuhitaji kuona wachezaji wa Yanga wakiishi kwa kuunga unga unapocheza timu kubwa ni lazima maisha yako yaonyeshe hivyo.

Mchezaji kulipwa mshahara wake ni haki yake tena amevumilia kwa muda mrefu, nadhani ni busara viongozi wa Yanga wakaa na wachezaji hawa na kuwalipa ili kurudisha morani ya timu mapema.

Dk Msolla umepokea jukumu la kuiongoza Yanga uje suala la mishahara ndiyo kipaumbele chako ili kupata kile mashabiki na wanachama wa Yanga wanataka kuona ubingwa ukirudi Jangwani.

Advertisement