Dilunga aanika siri za Sven

Friday February 14 2020

Dilunga aanika siri za Sven,KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Hassan Dilunga,Kocha Mbelgiji, Sven Vandernbroeck,

 

By Thobias Sebastian

KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Hassan Dilunga chini ya Kocha Mbelgiji, Sven Vandernbroeck amekuwa mtamu hadi anakera kwani, jamaa ameshjatupia kambani jumla ya mabao sita na kutoa pasi za mabao zaidi ya tatu kwa washambuliaji wengine jambo ambalo alishindwa kulifanya msimu mmoja zaidi akiwa katika kikosi hicho.

Simba akiwa chini ya Kocha Patrick Aussems, Desemba mwaka jana Dilunga alionekana mchezaji wa kawaida katika kikosi na alikuwa akiingia katika kipindi cha pili lakini chini ya Sven mambo yamekuwa tofauti, kwa sasa ndiye anayeiendesha na kuibeba timu hiyo.

Mwanaspoti lilimtafuta Dilunga na kueleza sababu tano zilizomfanya kuwa mchezaji muhimu wa kikosi cha kwanza akitoa pasi za mabao kwa wenzake na kufunga mabao mengi licha ya kucheza katika nafasi ya kiungo.

Dilunga alisema imekuwa kama bahati kwake kwani amekuwa akiyashika vizuri maelekezo ya Sven, ambayo humpatia, afanye pindi anapokuwa na mpira na amekuwa akifanya hivyo muda wote kwenye mechi.

Alisema jambo la pili ambalo Sven ameliongeza kwake ni kuwa makini katika sehemu mbili ya kwanza pale anapopewa mpira akiwa katika nafasi ya kiungo anatakiwa kutoa pasi sahihi ya kwenda mbele na wala si nyuma au pembeni lingine umakini anapokuwa katika eneo la hatari la timu pinzani.

“Hili la umakini kwangu limeweza kunisaidia kwa kutoa pasi za mabao na hata zile ambazo zinakwenda kuanzisha mashambulizi. Wakati huo nakuwa na umakini ambao umekuwa sababu ya kufunga idadi hiyo ya mabao ambayo naona ninayo kila sababu ya kuongeza zaidi mpaka mwisho wa msimu,” alisema.

Advertisement

“Jambo la tatu kila mchezaji anakuwa na bahati na kocha fulani, hilo ndilo limetokea kwangu chini ya Sven nimekuwa na bahati naye licha ya kunipa nafasi ya kucheza mara kwa mara lakini kila maagizo ambayo amekuwa akinipatia kwenda kuyafanya nimekuwa nikiyatimiza vizuri.

“Suala la nne ambalo nimelipata chini ya Sven amenipa hali ya kujiamini na kufanya vitu kwa uhuru uwanjani, kwani awali ilikuwa vigumu kuona nakaa na mpira zaidi na hata pale ambapo nikikosea nakuwa na uoga uliopitiliza, lakini kocha huyu amenijenga katika kujiamini na kufanya vitu ambavyo vipo ndani ya uwezo wangu na mpaka sasa kuweza kuwa bora,” alisema.

“Jambo la tano chini yake Sven najioni nitaendelea kufanya vizuri kwani imekuwa rahisi kwangu kuelewa mbinu na masuala ya kiufundi ambayo anahitaji, lakini ameweza kutujenga wachezaji wengi katika maeneo mengi ambayo tulikuwa hatuna na yalikuwa kama mapungufu kwetu jambo ambalo natamani aendelee kuwepo,” alisema Dilunga.

MSIKIE KOCHA SVEN

Sven amesema katika kikosi chake wachezaji wote ni wazuri jambo ambalo huenda hakulitegemea wakati alipokabidhiwa kuinoa timu hiyo.

Kwa maana hiyo kuzungumzia kiwango cha mchezaji mmoja mmoja si vyema bali wote waliokuwepo wanatimiza majukumu yao kulinga na nafasi ambazo wanacheza.

“Dilunga amekuwa mchezaji mahiri na kutimiza majukumu yake ipasavyo anapokuwa uwanjani, licha ya wakati mwingine kuonesha mapungufu lakini asingeweza kuonekana kuwa mzuri kwa kufunga idadi hiyo ya mabao na kucheza vyema bila ya kushirikiana na wachezaji wenzake,” alisema.

“Natamani kuona ushindani huo wa Dilunga uendelee kwa kila mchezaji ili anapopata nafasi ya kucheza aweze kufanya vyema kwani akifanya hivyo timu inakuwa rahisi kupata matokeo mazuri katika mechi zake na kufikia malengo ambayo imejipangia.

“Hakuna siri kwa Dilunga au wachezaji wengine wote, bali ni kufanyia kazi vizuri katika mechi kutokana na kuelekezana katika mazoezi,” alisema Sven ambaye atakiongoza tena kikosi hicho katika mechi ya ligi Jumamosi watakapocheza na Lipuli kwenye Uwanja wa Samora Iringa.

Advertisement