Dilunga,Bocco wawekewa Sh 200 milioni

Friday February 21 2020

Dilunga,Bocco wawekewa Sh 200 milioni,NAHODHA wa Simba, John Bocco ,Hassan Dilunga,Meddie Kagere,

 

By Olipa Assa

NAHODHA wa Simba, John Bocco sambamba na nyota wote akiwamo Hassan Dilunga na Meddie Kagere washindwe wenyewe tu, kwani mabosi wao wameamua kuwawekea mzigo wa maana mezani ili kuwajaza upepo na kuhakikisha wanaipa timu yao taji la tatu mfululizo la Ligi Kuu Bara.

Hali hiyo imeibua mzuka kuelekea kwenye mechi dhidi ya Biashara kesho Jumamosi ambapo mmoja wa vigogo wa benchi la ufundi ameliambia Mwanaspoti jana wachezaji wana mzuka sana na lazima cleansheet iendelee baada ya kufanya hivyo kwenye michezo mitatu iliyopita.

Simba ndiyo vinara kwa sasa wakiwa na alama 59 baada ya mechi 23 na mikononi wana michezo 15 kabla ya kumaliza msimu.

Kwa kutambua mechi za lala salama huwa zina changamoto wake na hasa baada ya kushtushwa na kipigo cha bao 1-0 walichopewa na JKT Tanzania, mabosi wa Simba waliamua kufanya jambo moja la maana la kukaa na benchi nzima la timu hiyo ili kuondoa tofauti za makocha, Sven Vanderbroeck na msaidizi wake, Seleman Matola.

Ndipo mabosi hao wakaamua kuwaita na kumaliza tofauti zao, kabla ya kuwageukia wachezaji wao na kukaa nao chini kujua wanatatizwa na kitu gani.

Ndipo nyota hao wakafunguka na kila mtu akitoa la moyoni, kisha mabosi wao wakawaambia watulie kwani, wanataka kuona chama lao linashinda kila mechi na wao watawaongezea bonasi walizokuwa wakipewa awali kila wanaposhinda.

Advertisement

Ipo hivi, awali viongozi wa Simba walikuwa wakitoa Sh 10 milioni kwa nyota wao kila wakishinda ili wagawane kulingana na walivyocheza, walivyokaa benchi na hata walivyokuwa jukwaani, lakini sasa wakawaongezea Sh 5 milioni na kufanya sasa wavune Sh 15 milioni kwa kila ushindi.

Jambo hilo linaelezwa limewaongezea morali wachezaji hao na kuanza kufanya mambo kwa kuwapiga Mtibwa Sugar mabao 3-0 wakiwa kwao Morogoro, kisha wakaifuata Lipuli na kuwalipua Uwanja wa Samora kwa bao 1-0 kabla ya juzi kati tena kuitandika Kagera Sugar jijini Dar es Salaam.

Kwa maana hiyo kwa mechi 15 zilizosalia kama kina Bocco na wenzake wataamua kukomaa nazo na kushinda zote watajihakikisha kuvuna Sh 225 milioni, wakianza na mechi yao ya kesho dhidi ya Biashara United.

Kama Bocco, Dilunga, Kagere na wenzao ambao wameonekana kuwa na uchu wa kupata ushindi kwa kila mechi, wataiwezesha Simba kujikusanyia jumla yua pointi 45 ambazo zikijumuishwa na walizonazo (59) watamaliza msimu wakiwa na pointi 104 itakayokuwa ni rekodi, licha ya kubeba taji.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya uongozi wa juu wa Simba zinasema bonasi hiyo ya Sh 15 milioni ilianza tangu mechi ya Mtibwa na itaendelea hadi mwisho wa msimu.

“Lengo la viongozi wa Simba ni kuhakikisha wanashinda mechi 15 zilizosalia ndio maana bonasi imeongezeka kwa wachezaji kutoka 10 mpaka 15 milionni,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Hii inaongeza morali kwa wachezaji kujituma kwa bidii maana watakuwa wanajua baada ya kazi watakuwa na kifuta jasho cha kufanya mambo yao yaende sawa.”

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa alikiri juu ya jambo hilo, lakini akisema ni siri yao juu ya kiwango kwa kudai klabu yao imekuwa na utaratibu wa kuwapa bonasi wachezaji wao kwa muda mrefu na kupata matokeo mazuri ni kutokana na wachezaji kutekeleza majukumu yao.

“Tunahitaji kuweka malengo na kushinda jambo ambalo tunaweza, tuna ratiba ngumu lakini tunaangalia jinsi gani tunaweza kuwasafirisha wachezaji wetu pasipo kuchoka sana maana tuna mechi za ugenini Mbeya na Shinyanga ambako tutacheza mechi ya Kombe la FA na Stand United.

“Yote haya tunayofanya huwa tunashirikiana na benchi la ufundi kuona ni namna gani tunawasaidia wachezaji wetu maana lengo ni kutwaa ubingwa wa ligi na FA maana tunataka kushiriki michuano ya kimataifa,” alisema Senzo ambaye ni raia wa Afrika Kusini mwenye uzoefu na soka la barani Afrika.

Advertisement