Diamond kumbadili Tanasha uraia kwa muda

Muktasari:

Tanzania na Kenya zitakutana kwa mara ya kwanza katika mashindano ya Afcon Alhamisi ya Juni 27 nchini Misri

Dar es Salaam. Mwanamuziki Diamond amesema atambadili uraia mpenzi wake mama kijacho Tanasha Donna Oketch kwa muda wakati wa mechi ya Afcon kati ya Tanzania dhidi ya Kenya.

Diamond amesema hayo Leo Juni 25, 2019 alipokuwa akitangaza kuzindua rasmi tamasha la Wasafi linalotarajia kuanza Julai 12, 2019.

Amesema wakati wa kuwania kufuzu kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ iliifunga timu ya mashemeji zake Uganda, lakini safari hii kwa mara ya kwanza atambadili uraia mpenzi wake huyo kutoka Kenya kwa kumshawishi ashangilie timu ya Tanzania.

“Atavaa jezi ya Tanzania na ataishangilia Taifa Stars, nitamshawishi, msiwe na hofu wifi yenu atawaunga mkono,” alisema Diamond.

Alipoulizwa kuhusu lini atafunga ndoa na mwanadada huyo baada ya kuwa ameshapata watoto na wanawake wawili tofauti na tayari huyo pia ni mama ijacho alijibu.

Badala ya kujibu alisema: “Subirini. Nimewaambia Julai 7, 2019 kutakuwa na tukio kubwa maeneo ya Mwenge Mwenge hapo, meza zitakuwa 10 tu meza tano zitauzwa Sh 500,000 kila moja.”