Degea kuuzwa dirisha hili,PSG kumpokea

Muktasari:

  • Msimamo wa De Gea katika suala la mkataba mpya limekuwa pigo kubwa kwa Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer ambaye amepania kukisuka upya kikosi chake baada ya kudorora msimu uliopita.

MANCHESTER,ENGLAND.NI mwendo wa mchakamchaka dirisha hili la uhamisho. Kwingine kunawaka moto. David de Gea amewapasua vichwa mabosi wa Manchester United baada ya kugomea ofa yao ya mwisho kabisa ya mkataba mpya klabuni hapo.

Sasa United hawana namna. Watalazimika kumuuza kipa huyo wa kimataifa wa Hispania ili waambulie chochote kabla ya kuingia mwaka wake wa mwisho wa mkataba na watajihatarisha kumwacha aondoke bure kama wasipomuuza sasa.

United imeshindwa kuafiki dau la mshahara analotaka De Gea kiasi cha Pauni 350,000 kwa wiki kitu ambacho PSG ipo tayari kumlipa kama akisaini kwao.

Kwa sasa PSG ina kiburi na ipo tayari kumnunua kwa Pauni 60 milioni tu na kama United itabisha, basi itakuwa tayari kusubiri mpaka mwishoni mwa msimu ujao imchukue bure kitu ambacho kinaiweka United katika presha ya kumuuza sasa.

Licha ya uhodari wake langoni kiasi cha kuaminika kuwa kipa bora kwa sasa duniani, dau hilo halitamwezesha kuwa kipa ghali duniani na mpaka sasa nafasi hiyo inashikiliwa na kipa, Kepa Arrizabalaga aliyenunuliwa na Chelsea kwa Pauni 75 milioni akitokea Atheltic Bilbao ya Hispania.

Msimamo wa De Gea katika suala la mkataba mpya limekuwa pigo kubwa kwa Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer ambaye amepania kukisuka upya kikosi chake baada ya kudorora msimu uliopita.

Mara nne katika misimu sita iliyopita, De Gea alichaguliwa kuwa mwanasoka bora wa msimu United lakini kuelekea mwishoni mwa msimu ulioisha alionekana kufanya makosa mara kwa mara huku kiwango chake kikihusishwa na masuala yake ya mkataba. Desemba mwaka jana, aliwaambia wachezaji wenzake wa Manchester United ataondola Old Trafford kama United haitaafiki madai yake katika mkataba mpya.

Solskjaer alifanikiwa kukibadilisha vyema kikosi cha United kilichodorora katika utawala wa Kocha Jose Mourinho lakini mara alipopewa kazi ya kudumu klabuni hapo, United ilianza kudorora. Sasa kuna uwezekano akaanza msimu ujao bila ya De Gea.

Mabosi wa United walitaka jibu la De Gea kabla ya kumalizika kwa msimu ulioisha hivi karibuni na sasa staa huyo amewapa jibu atalazimika kuondoka kama hawajaweza kufikia dau lake.

Tayari PSG imefanikiwa kuinasa saini ya staa mwingine wa United, Ander Herrera, 29, aliyechukuliwa bure wiki mbili zilizopita baada ya kumalizika kwa mkataba wake. PSG inapewa nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa wa Ufaransa msimu ujao, pia ina tamaa ya kufika mbali katika michuano ya Ligi ya Mabingwa baada ya kutolewa na Manchester United katika hatua ya mtoano msimu huu.

Kuna uwezekano mkubwa pambano la mwisho la msimu dhidi ya Cardiff ambalo United ilichapwa mabao 2-0 Old Trafford likawa la mwisho kwa kipa huyo wa Hispania na sasa United ina kazi ngumu ya kusaka mrithi wake.

Tayari ina kipa wa kimataifa wa Argentina, Sergio Romero pamoja na kipa, Dean Henderson aliyefanya mambo makubwa katika kikosi cha Sheffield United kilichopanda Ligi Kuu msimu huu lakini ni wazi huenda United ikalazimika kuingia sokoni kuziba pengo la De gea.

Katika maeneo ya ndani ya uwanja, Kocha Solskjaer ameanza kazi ya kukijenga kikosi hicho ambacho kimefikia dili la Pauni 15 milioni kumnunua winga mahiri wa Swansea, Dan James ambapo uhamisho huo utatangazwa muda wowote kuanzia leo