De Gea abebeshwa lawama Emirates

Muktasari:

Neville anaamini mazungumzo ya mkataba yanayoendelea kati ya De Gea na klabu yake Manchester United yanaweza kuwa yamesababisha kipa huyo mahiri wa Hispania kuondoka mchezoni wakati pambano hilo likiendelea.

LONDON ,ENGLAND.LILE bao la shuti kali la Granit Xhaka dhidi ya David de Gea juzi Jumapili limeanza kuzua gumzo. Anatafutwa mchawi. Mpira wake uliiingia katika nyavu za Manchester United katika namna ya kushangaza huku ukimuacha De Gea hana la kufanya.

Mashabiki walidhani upepo lakini beki wa zamani wa Manchester United, Gary Neville ambaye kwa sasa ni mchambuzi mahiri wa soka nchini England amemkamata mchawi wake. Anadai De Gea amejiroga mwenyewe katika bao lile.

Neville anaamini mazungumzo ya mkataba yanayoendelea kati ya De Gea na klabu yake Manchester United yanaweza kuwa yamesababisha kipa huyo mahiri wa Hispania kuondoka mchezoni wakati pambano hilo likiendelea.

Xhaka, staa wa kimataifa wa Uswisi alipiga shuti kali nje ya boksi la United katika dakika ya 12 ya pambano hilo na De Gea alikwenda upande wa kushoto huku mpira ukitinga upande wake wa kulia kwa mshangao wa wengi.

“Kitu cha kwanza unachosema mara baada ya kuona bao kama lile ni kudhani kuwa labda mpira uliguswa njiani. Hata hivyo haukuguswa. Ulikuwa ni ubovu wa David de Gea. Sijui namna sahihi ya kuelezea hilo. Xhaka alipiga shuti kali. Alimuona vizuri David de Gea. Alipiga shuti kali lakini siwezi kumtetea kipa. Kipa alifanya ovyo,” alisema Neville.

“Jinsi alivyojaribu kudaka alinishangaza. Alikwenda kushoto lakini hakuonekana kujishughulisha wakati mpira ulipokwenda kulia. Msimu huu hayupo katika ubora wake. Kumekuwa na kelele nyingi kuhusu mkataba wake. Inawezekana anasikia kelele nyingi masikioni mwake,” alisema Neville.

Naye staa wa zamani wa Liverpool na timu ya taifa ya England, Jamie Redknapp alikubaliana na Neville huku akisema “Lugha yake ya mwili inashangaza na nakubaliana na wewe Gary kwamba inabidi aongeze juhudi langoni.”

Staa mwingine wa zamani wa Liverpool, Graeme Souness alidai tatizo kubwa la United katika pambano hilo lilikuwa viungo wake watatu, Fred, Nemanja Matic na Paul Pogba ambao hawakuwa katika ubora wao na hawakuwa na kasi.

“Haikuwa United ambayo tumeiona katika wiki za karibuni. Sababu kubwa ilikuwa eneo la kiungo. Hakukuwa na kasi. Fred, (Nemanja) Matic na (Paul) Pogba. Hawakumkaribia yeyote. Nimekuwa nikimkosoa Granit Xhaka mara nyingi lakini nadhani alikuwa bora sana. Alifanya kila kitu kwa usahihi. Tazama bao lake, Matic hakumkimbilia kabisa. United imepambana sana katika wiki za karibuni. Dhidi ya PSG walitumia sana nguvu lakini sio katika mechi hii,” alisema Souness.

Staa mwingine wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher alikataa hilo na kudai Manchester United ilicheza vizuri isipokuwa ilipoteza nafasi zao huku pia Arsenal ikifunga mabao mawili ya bahati.

“Sidhani kama Manchester United imecheza ovyo. Waliruhusu bao la bahati mbaya na penalti ambayo pengine haikupaswa kutolewa. Walipata nafasi nyingi na ni suala la kuzitumia vizuri au vibaya,” alisema Carragher.

Na sasa Arsenal inakamata nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa imeiondoa Man United ambayo kabla ya mechi ya juzi ilikuwa inashika nafasi hiyo. Wanasimama juu ya United kwa tofauti ya pointi mbili ikiwa na pointi 60 wakati United ina pointi 58.

Chelsea yenye mechi moja mkononi inashika nafasi ya sita baada ya kubanwa mbavu na Wolves kwa kutoka sare ya 1-1 katika pambano lililofanyika Stamford Bridge muda mchache kabla ya Arsenal kuichapa United.

Arsenal pia inasimama nyuma ya Tottenham inayoshika nafasi ya tatu kwa tofauti ya pointi moja tu huku wapinzani wao hao wa jadi wa London Kaskazini wakiwa na pointi 61. Arsenal ingeweza kushika nafasi ya tatu kwa sasa kama si mshambuliaji wao, Pierre-Emerick Aubameyang kukosa penalti katika dakika za mwisho za pambano lao Jumamosi iliyopita. Pambano hilo lilimalizika kwa sare ya 1-1.