De Bruyne hana shaka kuhusu Lionel Messi

MANCHESTER, ENGLAND. MMESIKIA? Kiungo wa Manchester City, Kevin De Bruyne amesema klabu yake ina wachezaji wengi na wenye ubora ambao wanaweza kupigana na kuhakikisha inafanya vizuri hivyo kusajiliwa ama kutosajiliwa kwa Lionel Messi hakumpi wasi wasi wowote na hajali kabisa kuhusu jambo hilo.

Man City ilikuwa kwenye harakati za kuisaka saini ya mchezaji huyo wa Barcelona anayeshikilia rekodi ya kushinda tuzo za mchezaji bora wa dunia mara sita, katika dirisha lililopita, lakini ilikwama kwenye kutoa kiasi cha pesa ambacho Barca walikuwa wanakihitaji baada ya kile kipengele ambacho kingemruhusu fundi huyo kuondoka bure kuwa kimeisha muda wake.

“Sijali kuhusu hilo, niwe tu muwazi, kama atakuja litakuwa ni jambo jema na kama hatokuja ni jambo zuri pia kwa kuwa kuna wachezaji wengi wazuri ambao najisikia furaha kucheza nao na wanaweza kuifanyia timu makubwa,” alisema De Bruyne.

Fununu za Messi kuwa anaweza kutua Man City katika dirisha lijalo la majira ya joto zimeongezeka baada ya kauli alizozitoa Ofisa Mtendaji wa klabu hiyo Omar Berrada katika siku za hivi karibuni alipoulizwa kuhusiana na uwezekano wa mchezaji huyo kusajiliwa katika kikosi chao.

“Ni miongoni mwa wachezaji wachache ambao wana vipaji vya kushangaza sana, pia anaweza kucheza kwenye klabu yoyote duniani na akaonyesha kiwango kikubwa pia na mafanikio ya nje na ndani ya uwanja kwa klabu husika,” alisema Berrada.

“Huyu sio mchezaji bora tu wa duniani kwa sasa, bali ni mchezaji bora wa kizazi chake na nafikiri hakuna klabu ambayo haitamani kuwa naye inapopata nafasi ya kufanya hivyo,’’ aliongeza.

Berrada alisema Messi mwenyewe aliichagua Man City kama timu ambayo anahitaji kuchezea na wao kama viongozi walifarijika sana na jambo hilo na walikuwa tayari kumsajili lakini dili lilikuja kubadilika katika wiki mbili za mwisho.

‘’Siwezi kusema dirisha lijalo la majira ya kiangazi nini kitafuata, lakini ninachoamini Messi ni mchezaji mzuri kuwekeza kwake.”