MTAA WA KATI : Dani wa Emirates anavyomuumbua Zidane wa Bernabeu

Wednesday September 11 2019

 

By Said Pendeza

DENIS Suarez ameenda. Dani Ceballos amekuja. Wa kwanza ametoka Nou Camp, wa pili ametokea Bernabeu. Wote wametua Emirates kwa mkopo.

Denis alitumikia muda wake Emirates kuanzia Januari hadi Juni, hakuwa na jipya. Hakumshtua Unai Emery na wala huko Nou Camp hawajashtuka pia. Dani amekuja wakati huu Emirates.

Wiki chache sana zimepita tangu alipoanza utumishi wake akiwa na uzi wa Arsenal. Wawili hao wote walikwenda kumtumikia Mhispaniola mwenzao, Emery huko Emirates kwa mkopo. Dani hashikiki, kazi yake imekuwa mzuri kuliko matarajio.

Huduma bora Emirates imemfanya Dani kurudi Hispania kuitumikia La Roja. Anachokifanya Dani huko Emirates, kina madhara makubwa Bernabeu.

Wale waliomwona hafai akiwamo Zidane na kumtoa kikosini, wanatafuta mahali pa kuficha sura zao kwa sasa. Sawa kitu ambacho wanaweza kujitetea kwamba hakuondoka moja kwa moja Bernabeu, atarudi.

Dani hakuna ubishi ni kipenzi cha rais, Florentino Perez. Lakini, shida ilikuwa Zidane, alimwona hafai. Pengine anachokifanya Dani kwa sasa ni kumkomesha Zizou, kwamba amekosea kwenye uamuzi wake wa kumwondoa.

Advertisement

Zidane na Dani shida picha haziendi tu. Jambo hilo linawafanya wengi waamini kama Mfaransa huyo ataendelea kuwa Kocha Bernabeu, basi huenda Dani asitinge tena mwilini mwake uzi wa Merengues.

Akabaki zake Emirates kuendelea kuwa mshika bunduki. Madrid imeshinda mechi moja na kutoka sare mbili kwenye La Liga msimu huu.

Kikosi chao kikikosa ubunifu mkubwa ndani ya uwanja, jambo linalowafanya mashabiki wa timu hiyo, kuhoji Zidane alitumia akili ya watu kumwondoa Dani kikosini.

Madrid inaonekana kuwa hofu. Sehemu kubwa ya viungo wake, umri umekwenda sana. Luka Modric, Casemiro, Toni Kroos wote wamechoka.

Zidane alihitaji kuwa na damu moto kama Dani kwa wakati huu kuifanya timu hiyo kuwa na uhai kwenye sehemu hiyo ya katikati ya uwanja. Amemwaacha ameondoka.

Lakini, taarifa zinamfikia huko huko Madrid, kwa sababu vyombo vya habari za Hispania havikomi kumwaandika Dani kila wiki kwa kile anachokifanya kwenye Ligi Kuu England akiwa na uzi wa Arsenal.

Dani ameshakuwa kipenzi cha mashabiki huko Arsenal, kipenzi cha kocha Emery. Wahispaniola wanafahamu vyema uwezo wa Dani. Florentino alipambana sana kuwashinda Barcelona kwenye kunasa saini yake.

Julen Lopetegui na Santiago Solari wote walipoanza maisha yake Bernabeu, walimweka Dani kwenye kwenye timu. Hata Luis Enrique alimfanya Dani kucheza mechi yake kwanza kwenye kikosio cha La Roja.

Kwa kifupi tu, huko Hispania, Dani wanamwona kuwa ni kiungo bora wa kizazi chake kwa sasa baada ya kupita kile cha kina Andres Iniesta, Xabi, Fabregas na wengineo.

Lakini, maisha yake chini ya Zidane hajawahi kuwa mepesi. Kama Zidane asistaafu, pengine kwa sasa Dani asingekuwa mchezaji wa Los Blancos tena, angeshaondoka kitambo.

Alimtia tu kwenye benchi bila ya sababu na kuendelea kuwatumia kina Modric hata katika kipindi ambacho walikuwa hovyo uwanjani.

Lakini, sasa amepata nafasi ya kumwonyesha kile ambacho amekuwa akiweka ngumu kukielewa, uwezo wake wa kuucheza mpira. Ujeuri tu ndio utakaofanywa na Zidane kuhusu kukubali vitu vya Dani uwanjani.

Huko Emirates, kwa haraka sana, mashabiki wameshamsahau Aaron Ramsey. Dani huyo. Alihitaji wiki chache tu kupafanya Emirates kuwa mahali pa makazi yake ya muda mrefu.

Bila shaka akiendelea kwenye ubora huo, Emery atahitaji kubaki na huduma yake kwa muda mrefu, kufanya kiungo yake kuwa ya vijana watupu sambamba na Matteo Guendouzi.

Ndiyo hivyo, Dani ametua na kuifanya jezi Namba 8 kuizoea mwili wake kama amekuwa akiivaa kwa muda mrefu.

Tofauti na ilivyokuwa kwa Denis, ambaye pengine kwa sasa hatahitaji kukumbuka kabisa kitu kuhusu Emirates.

Advertisement