Dakika 33 uwanjani zilivyobadili maisha ya Niyonzima

Muktasari:

  • Kasi yake ya kumiliki mpira, chenga za maudhi na kutoa pasi za uhakika zinazofika kwa mlengwa, ziliwavuruga mabeki wa AS Vita na kuruhusu bao la kiungo wa kimataifa wa Zambia, Clatous Chama zikiwa zimebaki dakika tatu kabla ya mpira kumalizika.

Dar es Salaam.Dakika 33 zimebadili maisha ya kiungo wa kimataifa wa Simba na timu ya Taifa ya Rwanda ‘Amavubi’, Haruna Niyonzima.

Ndio. Kiungo huyo alibadili upepo alipoingia dakika ya 57 katika mchezo wa kimataifa wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita ya DR Congo.

Niyonzima ndiye alikuwa nyota wa mchezo huo baada ya kuingia kujaza nafasi ya mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi.

Awali, Simba ikiwa imezidiwa huku ubao wa matokeo ukionyesha sare ya bao 1-1, Kocha Patrick Aussems alifanya uamuzi mgumu wa kumtoa mshambuliaji na kumuingiza kiungo.

Mabadiliko hayo yaliibua minong’ono ya mashabiki walioanza kuponda uamuzi huo wakidai Niyonzima hakuwa mtu sahihi wa kuingia katika mchezo huo.

Hata hivyo, Aussems alithibitisha kile anachokifanya alikuwa na uhakika nacho kwani muda mfupi baada ya Niyonzima kuingia, alibadili sura ya mchezo kwa asilimia 90.

Kasi yake ya kumiliki mpira, chenga za maudhi na kutoa pasi za uhakika zinazofika kwa mlengwa, ziliwavuruga mabeki wa AS Vita na kuruhusu bao la kiungo wa kimataifa wa Zambia, Clatous Chama zikiwa zimebaki dakika tatu kabla ya mpira kumalizika.

Haikushangaza baada ya mchezo kumalizika, mashabiki waliokwenda uwanjani kumbeba Niyonzima badala ya Chama aliyeipeleka Simba katika hatua ya robo fainali.

Itakumbukwa kwamba kabla ya mchezo huo, Niyonzima hakuwa katika maelewano mazuri ya Aussems na uongozi wa klabu hiyo kutokana na sababu mbalimbali.

Niyonzima alisugua benchi muda mrefu katika mechi za ligi akiuguza majeraha na suala lake la mkataba ambalo liliibua sintofahamu na uongozi wake.

Msimu miwili iliyopita Niyonzima alisajiliwa na Simba akitokea Yanga na uhamisho wake uliwaduwaza mashabiki wa klabu yake ya zamani ambapo alikuwa kipenzi chao.

Niyonzima mbali na kushindwa kuwa sehemu ya maandalizi ya ligi chini ya Aussems, pia alikuwa na majeraha yaliyomuweka nje muda mrefu mpaka msimu ulipoanza na alikosa idadi kubwa ya mechi.

Wiki moja kabla ya mechi ya mzunguko dhidi ya Yanga, Salim Abdallah ‘Try Again’ alimruhusu Niyonzima kwa mara ya kwanza kufanya mazoezi  Uwanja wa Boko Veterani.

Niyonzima anasema amepitia kipindi kigumu msimu uliopita kutokana na sababu mbalimbali yakiwemo majeruhi yaliyomuweka nje ya uwanja muda mrefu.

“Kabla ya kuanza msimu wenzangu walikuwepo Uturuki mimi nilikuwa naumwa, pia nilikuwaa na matatizo ya kifanikia ambayo yalichangia kushindwa kucheza vizuri katika kiwango changu.

“Wakati namaliza matatizo ya kifamilia nilikutana na changamoto ya kutokuwa vizuri na uongozi wangu wa Simba iliyochukua muda mpaka kumalizika. Nilijiunga na timu wanzangu wakiwa katika kiwango cha juu katika mashindano,”anasema Niyonzima.

Nahodha huyo wa zamani wa Rwanda, anasema haikuwa kazi rahisi kurejea katika ubora wake kutokana na misukosuko mingi aliyopitia msimu uliopita.

Niyonzima ametoa ahadi kwa mashabiki wa Simba msimu ujao utakuwa wa mafanikio kwake kwa kuwa amejipanga kikamilifu kuwania namba katika kikosi cha kwanza.