Corona yatibua mashindano Ngajilo Super Cup Iringa

Muktasari:

Mashindano hayo yanashirikisha timu 32, bingwa wake anapata kombe na fedha Sh1milioni taslimu, mshindi wa pili shilingi laki tano, mshindi wa tatu atapata laki tatu, huku wito ukitolewa kwa Watanzania kujilinda na maambukizi ya corona.

IRINGA. Kamati ya Mashindano ya Ngajilo Super Cup imeahirisha mashindano hayo kutokana na agizo la serikali la kuzuia mikusanyiko kwa sababu ya tishio la kusambaa kwa ugonjwa wa corona.

Akitangaza kuahirisha mashindano hayo mratibu wa Davis Eapalila alisema kamati hiyo inaunga mkono juhudi za serikali katika mapambano ya ugonjwa huo na kutumia nafasi hiyo kuzijulisha klabu kuwa mashindano hayo yanatarajia kuzinduliwa ifikapo Mei Mosi mwaka huu.

Davis alisema pamoja na matukio mengi yanayotokea tayari walishapata kibali cha kuendesha mashindano hayo, kwa bahati mbaya kutokana na janga la ugonjwa corona na matamko ya serikali kuzuia mikusanyiko na tamko la TFF kuzuia mashindano yote kwa siku 30.

Akizungumza uamuzi huo nahodha wa Don Bosco, Damas Thomas alisema ili ugonjwa wa corona usisambae ni lazima tuache mikusanyiko, na ukiwa katika timu lazima ufanye mazoezi kwa pamoja jambo ambalo litasababisha mkusanyiko.

“Wachezaji tumeipokea vizuri na pia tunaona tumeongezewa muda zaidi wa kufanya mazoezi ya mmoja mmoja kwa sababu haturuhusiwi kukutana wengi ama kufanya mazoezi ya pamoja hivyo tunaomba mungu janga hili lipite salama na tuendelee na michezo”alisema

Mashindano hayo yanashirikisha timu 32, bingwa wake anapata kombe na fedha Sh1milioni taslimu, mshindi wa pili shilingi laki tano, mshindi wa tatu atapata laki tatu, huku wito ukitolewa kwa Watanzania kujilinda na maambukizi ya corona.