TASWIRA YA MLANGABOY : Chuji amenikumbusha kilio cha mtu mzima

Saturday July 13 2019

 

By Andrew Kingamkono

UKIONA mtu mzima mamaa…analia mbele za watu ujue kuna jambo…. Ukiona mtu mzima mamaa… analia mbele za watu ujue kuna jambo…’ hiki ni kibwagizo cha wimbo wa Msondo Ngoma unaoitwa Kilio cha mtu mzima.

Hakuna ubishi utakapomuona mtoto akilia barabarani au mbele za watu huwezi kushtuka kwa lolote zaidi ya kujaribu kumnyamazisha kwa kumbembeleza, lakini utakapoona mtu mzima akitokwa na machozi mbele za watu kuna maswali mengi utakuwa unajiuliza.

Maswali ya kawaida tu ukiona mtu mzima analia utajiuliza je huyu bwana kafiwa, anaumwa, ameibiwa na mengine ya aina hiyo.

Nimekumbuka wimbo huu wa Msondo baada ya hivi karibuni kusikia kauli ya kiungo mkongwe wa zamani wa Simba, Yanga na sasa Coastal Union, Athuman Idd ‘Chuji’ akiwataka wachezaji chipukizi kuuheshimu mpira.

Chuji anasema milango ya mafanikio kwa sasa ipo wazi, jambo analowasisitiza chipukizi kuona fursa hiyo kwa faida ya maisha yao na taifa la Tanzania.

“Nimejifunza kitu kikubwa kwamba unavyolichukulia soka ndivyo linavyokupeleka, hivyo madogo wajaribu kuona uzito na heshima ambayo ipo kwenye soka watafika mbali, waepukane na vitu ambavyo havina maana kwao,” anasema Chuji, mwisho wa kunukuu.

Advertisement

Nimemuelewa Chuji, nilitamani na wachezaji chipukizi na nyota wa sasa wangekuwa na akili ya kumwelewa kiungo huyo.

Unapotaja viungo bora waliowahi kutokea nchini hakuna ubishi jina la Chuji huwezi kulikosa kabisa, ni kijana aliyeibukia katika timu ya Polisi Dodoma na baadaye Simba kabla ya kutimkia Yanga.

Chuji katika ubora wake alikuwa kiungo aliyetimia kila idara, alikuwa mzuri katika kucheza mipira ya juu, chini achilia mbali uwezo wake wa kupiga pasi ndefu na kupiga mashuti na ufungaji.

Unapokwenda uwanjani kuitazama Yanga ukimuona Chuji basi unajua leo Mrisho Ngassa atakimbia vya kutosha kwa sababu ya pasi mororo za uhakika kutoka kwa kiungo huyo. Maisha yake ya nje ya uwanja hayakuwa ya mchezaji aliyejitambua kivile maana yalitawaliwa na usera mwingi na kushindwa kuheshimu kazi yake ya mpira ambayo yamemfanya leo awe alipo.

Kauli yake ya kuwataka wachezaji vijana wa sasa waheshimu mpira ni wazi kuna nyakati nyingi ngumu anapitia katika maisha yake ya kawaida. Leo Chuji si Chuji tena, hawezi kucheza kwa kiwango kile, amepoteza mashabiki, amepoteza washikaji na wengi waliobaki wanamuona kama mtu asiyekuwa na dira maishani kwa sababu miguu yake haina ubora ule kwa sababu umri umekwenda. Akili inataka, lakini mwili unakataa.

Rafiki yangu Chuji anawangalia wadogo zake kina Ibrahim Ajibu, Gadiel Michael, Deogratus Munishi ‘Dida’ na wengine wengi wanashindwa kutumia vizuri nafasi zao wanazopata sasa, wanakaa kuangalia jinsi ya kubadilisha mitaa ya Kariakoo leo Msimbazi kesho Jangwani na Twiga.

Naona jinsi Chuji anavyotokwa na machozi kwa sababu anajua mwisho wa yote anawakumbusha vijana wakiheshimu mpira utawapa maisha mazuri baadaye kwa sababu muda wa kucheza soka kwa Tanzania ni miaka mitano na mtu akijitaidi sana ni miaka 10.

Siyo Chuji tu, walioshindwa kuheshimu vipaji vyao wapo wengi wakiwamo kina Haruna Moshi ‘Boban’ na Mrisho Ngassa kwa nyakati tofauti, na wao watakuwa wanajutia ujana wao na kushindwa kuheshimu soka. Leo wamekuwa watu wa kuomba hisani ili wasajiliwe na Yanga maisha yaende.

Ukiwatazama Thomas Ulimwengu, Himid Mao ndipo utakapojua maana halisi ya kuheshimu soka. Ulimwengu na Himid si wachezaji wenye vipaji vikubwa au kulingana na Chuji hata robo.

Himid na Ulimwengu wamejua hilo mapema wameamua kuheshimu kazi yao na kucheza kwa kujitoa, leo hii wanacheza soka la kulipwa Misri na Algeria. Wale wenye vipaji wamebaki nyumbani wanauza sura. Naamini Mbwana Samatta, Saimon Msuva, Chipukizi Kibabage ni miongoni mwa wachezaji wachache wa Tanzania walioamua kuheshimu mpira na kuifanya kuwa kazi yenye maana kwa maisha yao.

Wachezaji hao wanaocheza kwa kujituma huko duniani hata watakapostaafu watakuwa na maisha bora na kuepuka kwenda kuliakulia TFF kuomba msaada kwa Watanzania.

Ni lazima wachezaji wetu wajifunze kufanya uwekezaji katika masuala mbalimbali ya kijamii hasa katika vipindi vyao wanapokuwa juu na kupata pesa nyingi kwa muda mfupi.

Angalia Lionel Messi na Cristiano Ronaldo ni wachezaji wenye uwekezaji mkubwa katika hoteli na vitega uchumi mbalimbali wakijiandalia vyema maisha baada ya soka kwa sasa wakiwa na miaka kati ya 33-35.

Wachezaji wetu wanapaswa kujifunza kitu kwa kauli hii ya Chuji - mtoto mtukutu anapozungumza neno la busara kwa kiwango hiki ni wazi kuna jambo zito ameliona.

Kweli Ukiona mtu mzima analia mbele za watu ujue kuna jambo.

Advertisement