Christian Bella, Chaz Baba wafunika

Sunday August 11 2019

 

By RHOBI CHACHA

USIKU wa kuamkia leo wapenzi wa burudani waliofurika ndani ya ukumbi wa Kilimani Dodoma, walipata uhondo bab’kubwa kwenye onyesho la Sakata Dansi lililokutanisha bendi nane na kusindikizwa na wanamuziki Christian Bella,Chaz Baba na Kalala Junior.

Burudani hiyo iliwafanya mashabiki wapagawe na kujimwaya uwanjani mwanzo-mwisho huku  zikichezwa staili mbalimbali zilizokuwa zikinogesha usiku huo.

Bendi zilizotoa burudani kwenye onyesho hilo ni Sky Melodies, PMB, TNC, Gold Musica, Dodoma Extra, Delemba, Saki Stars na WK.

Aidha sambamba na burudani hiyo, mgeni rasmi alikuwa Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde aliyeambatana na viongozi wengine kama Katibu wa Chamudata Hassan Msumari, Mariam Ditopile Mbunge wa viti maalum kwa tiketi ya CCM  Mkoani Dodoma.

Pazi la burudani lilianza kufunguliwa na bendi ya TNC majira ya saa 3 usiku, ambapo iliweza kutumbuiza muda mwingi sebene  na kuwashawishi watu waliokuwa kwenye viti kuinuka kucheza.

Ilipofika saa 4:45 alipandishwa kwenye steji mh Mavunde na Katibu wa Chamudata Hassan Msumari kwa ajili ya kusalimia watu waliohudhuria katika onyesho hilo, hapa Mshehereheshaji wa onyesho hilo Mc Petit aliwaambia washindane kucheza sebene viongozi hao.

Advertisement

Shangwe za makofi na miluzi vililipuka ukumbini,kwa vile Mavunde alivyoonyesha uhodari wake wa kukata mauno.

Burudani iliendelea, pale mshereheshaji wa onyesho aliipandisha bendi ya Dodoma Extra ambao walionyesha ubunifu wa kuvaa mavazi ya  asili ya kabila la Kigogo.

Baada ya hapo PMB bendi ilipanda jukwaani ikifuatiwa na WK, Saki Stars, Belemba na Golden.

Ikiwa bendi husika hazijamalizika, alipanda jukwaani mwimbaji Christian Bella ambaye aliteka mashabiki kwa kuimba nyimbo zake kama Nani Kama Mama, Msaliti, Nagharamia, Safari Sio Kifo.

Bella kabla hajashuka jukwaani aliwaita wanamuziki Chaz Baba na Kalala  Junior na kuimba wote wimbo wa kuachwa wa Mapacha wa tatu.

Bendi ya Sky Melodies ilifuata kuimba nyimbo zake kama penzi kihozi na Shukrani kwa wazazi.

Aidha bendi ya TNC ilirudi jukwaani kwa mmara ya pili na kuimba wimbo wa 'kwetu' ulioimbwa kwa Lugha ya kigogo na ndio waliofunga pazia la burudani majira ya saa 9 na dakika 58.

Tamasha hili ambalo lina lengo la kuinua muziki wa dansi, litakuwa likifanyik kila mwaka mjini hapo Dodoma.

Advertisement