Chirwa, Ngoma waula Azam

Muktasari:

  • Akizungumzia maisha mapya ndani ya Azam, Ndayiragije alisema yupo tayari kukabiliana na changamoto mpya.

KABLA hata msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2018/2019 haujamalizika, Azam FC ilipambana kuwapa mikataba mipya mastaa wake hasa wale wa kigeni huku wakiwa hawajakamilisha mchakato wa kumpata kocha mkuu.

Miongoni mwa nyota walioongezewa mikataba ni Donald Ngoma, Daniel Amoah na Yakubu Mohamed huku pia ikiwa mbioni kuongeza mkataba wa mshambuliaji Obrey Chirwa.

Kabla ya hapo Azam FC ilipanga kutotoa mikataba mipya kwa wale ambao mikataba ya kwao imemalizika hadi pale watakapopata kocha mpya lakini ghafla imebadili uamuzi huo na kuanza kuwaongezea wachezaji wake mikataba.

Hata hivyo, juhudi zote hizo za Azam kumbe ni sehemu ya utekelezaji wa mipango ya kocha mpya ambaye ilikuwa kwenye mazungumzo naye, yaliyokamilika jana, Etienne Ndayiragije waliyemnasa kutoka KMC ya Kinondoni jijini.

Kocha huyo aliyesaini mkataba wa miaka miwili na kutambulishwa rasmi na klabu hiyo jana, amefichua haitaji mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha Azam FC na badala yake anaridhika na wachezaji waliopo.

Akizungumzia maisha mapya ndani ya Azam, Ndayiragije alisema yupo tayari kukabiliana na changamoto mpya.

Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’ alisema wanaamini kocha huyo atawapa mataji pamoja na kuendeleza mfumo wa soka la vijana.

“Kwa niaba ya bodi ya timu, nachukua fursa hii kumkaribisha kocha Etienne. Tumefanya utafiti wa kutosha tukabaini kuwa yeye ni mtu sahihi wa kuwa kocha mkuu wa Azam.

Kikubwa sisi kipaumbele chetu ni kupata kupata kila kombe tunaloshiriki na ndio maana huwa tunafanya vizuri hata kwenye Kombe la Mapinduzi lakini pia ni kocha ambaye anatoa fursa kwa vijana,” alisema Popat.