Chilunda atasepa na kijiji

Saturday October 03 2020
chilunda pic

MSHAMBULIAJI wa Difaa Al Jadid, Mtanzania Saimon Msuva amesema kwa aina ya uchezaji wa Shaaban Chilunda anayejiunga na timu ya D’oujda ya Morocco, atang’ara na kuwa na thamani kubwa.

Huu ni mwaka wa nne kwa Msuva kucheza huku Morocco ikiwa ni tangu 2017 akitokea Yanga, ambapo alisema amepata uzoefu wa aina ya uchezaji wa ligi hiyo inayotumia akili na mbinu kama anavyocheza Chilunda.

Alisema endapo Chilunda akifanya juhudi, basi ni rahisi kung’ara Morocco ambako wanatumia akili na sio nguvu kama Tanzania.

“Aina ya uchezaji wa Chilunda amefanya chaguo sahihi kuja kucheza Ligi Kuu ya Morocco kwani anang’ara sana kama ataelekeza nguvu kupambana ili kufikia malengo yake,” alisema Msuva.

“Ingawa sehemu nilipo na anakokwenda yeye kwa basi ni saa nane, lakini ligi ndio ileile, ninachofurahia ni kwamba Watanzania tunazidi kupanua wigo wa kuwa wengi kucheza ligi ya Morocco, hili litasaidia kwenye timu yetu ya taifa kuwa na vionjo tofauti.”

Chilunda atakuwa Mtanzania wa nne kucheza ligi ya Morocco atakakoungana na Msuva, Nickson Kibabage na Edward Makaka ambaye anaichezea Moghreb Tetouan. Hii ni timu ya tatu ya nje Chilunda kuichezea ambapo alianzia Tenerife aliyojiunga nayo 2018 kwa mkopo, Izarra alikocheza kwa mkopo 2019 na sasa ni mchezaji wa D’oujda. Tayari Azam FC imetoa baraka kwa Chilunda kujiunga na timu hiyo mpya.

Advertisement
Advertisement