Chilunda amfuata Msuva Morocco

MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Shaaban Idd Chilunda anajiandaa kumfuata nyota wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva kwenye Ligi Kuu ya nchini Morocco baada ya kumalizana na klabu ya Mouloudia Oujda.

Mmoja wa watu wa karibu wa Chilunda aliipenyezea Mwanaspoti kwamba, mshambuliaji huyo aliyewahi kucheza Hispania katika klabu ya CD Tenerife, licha ya kupata dili nyingi, lakini ameamua kwenda Oujda na tayari wameshamalizana nao.

“Chilunda alikuwa na ofa za Sauzi (Afrika Kusini), Misri na hii ya Morocco, naye ameomba viongozi wamruhusu aende Morocco na uzuri wamemsikiliza, licha ya kuwa na mkataba Azam,” chanzo hicho kilisema, huku uongozi wa Azam nao ukithibitisha jambo hilo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’ amethibitisha kwamba kila kitu kimemalizika.

“Chilunda alikuwa bado ana mkataba na Azam, ila kwa upande wa klabu na klabu kila kitu kipo sawa, bado yeye mwenyewe na klabu husika tu kukubaliana,” alisema Popat.

Klabu hiyo ya Oujda ipo nafasi ya nne kwa sasa katika msimamo wa Ligi Kuu ya Morocco ikiwa na pointi 41 baada ya kucheza mechi 25, imeshinda mechi 10, sare 11 na kupoteza nne.