Cheki tizi la Man United lilivyonoga huko Dubai

Thursday January 10 2019

 

DUBAI, FALME ZA KIARABU.HUKO kwenye kambi ya mazoezi ya Manchester United kumenoga kinoma. Kocha, Ole Gunnar Solskjaer amewapa uhuru wachezaji wake kufurahia maisha ya kuichezea Man United.

Mastaa wa Man United kwa sasa wanaishi maisha wanavyotaka.

Ndio maana hata juzi tu hapo, mastaa wa timu hiyo wakiongozwa na Romelu Lukaku, Anthony Martial na Andreas Perreira walipata nafasi ya kwenda kwa mchoma nyama maarufu huko Dubai, Salt Bae.

Man United kwa sasa imeweka kambi ya mazoezi huko Dubai, Falme za Kiarabu, ikifuata hali ya hewa ya joto kufanya mazoezi kujiandaa na mechi zijazo, ikiwamo dhidi ya Tottenham Hotspur kwenye Ligi Kuu England wikiendi ijayo.

Kambi yake huko imenoga kwelikweli, ambapo mastaa wa timu hiyo wote wakionekana kufurahia mazoezi yao. Mastaa wote kama Antonio Valencia, Alexis Sanchez, Eric Bailly na Juan Mata wamekuwa wakifurahia hali ya joto ya eneo hilo.

Kocha Solskjaer amekuwa na kundi kubwa la wachezaji wake, akiwamo Eric Bailly, ambaye alionyeshwa kadi nyekundu kwenye mechi iliyopita ya ligi, lakini Jesse Lingard akiwachekesha wenzake wa kupiga selfie kwa kutumikia kamera ya kawaida.

Marcos Rojo na Fred hawakuonekana kwenye kambi hiyo na wenzao, wakati wakijifua kwenye viwanja vya Nad Al Sheba Sports Complex.

Alipoulizwa Kocha Solskjaer kuhusu mastaa hao alisema: “Marcos Rojo amerudi nyumbani kwa sababu ya majeraha yake kuwa makubwa tofauti na ilivyofikiriwa. Fred anatarajia mtoto.”

Kwenye kikosi cha kwanza, mastaa hao wawili Rojo na Fred ndio wanaompunguzia hesabu Kocha Solskjaer katika mkakati wake wa kuwapa mambo matamu wachezaji wake wote, huku akiwambia ni afya kwa wachezaji wa timu moja kulumbana ndani ya uwanja kama ikionekana mmoja hatimizi majukumu yake ipasavyo.Kuondoka kwa Jose Mourinho, maisha ya wachezaji yameonekana kuwa na furaha zaidi kwa sasa.

Advertisement