Chama alivyotamba kwenye tuzo

KESHOKUTWA Ijumaa Agosti 7, 2020 pale kwenye Ukumbi wa Mlimani City kutakuwa na shughuli ya utoaji tuzo kwa wachezaji katika nyanja tofauti kwa msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara.

Awali Shirikisho la Soka nchini (TFF) lilitoa orodha ya wachezaji 30 wanaowania tuzo hizo na juzi Jumatatu orodha ya pili ya wachezaji 15 waliopita ilitolewa.

Mwanaspoti linakuchambulia nafasi hizo ambazo zimegawanywa katika vipengele 10 ambavyo ni mshambuliaji, beki, kiungo, kocha, nidhamu, waamuzi, mchezaji bora, bao bora na chipukizi.

MSHAMBULIAJI BORA

Majina pekee matatu ya washambuliaji yaliyotangazwa katika orodha hiyo ya mwisho ni Luis Miquissone wa Simba, Sadallah Lipangile (KMC) na Patson Shikala (Mbeya City).

Ni orodha ambayo imetawaliwa zaidi na Simba ambayo imetoa washindani katika vipengele vitano tofauti huku Yanga wakitoa mshindani katika kipengele kimoja kama ilivyo kwa Azam FC.

Yaliyotokea mara nyingi

Mabeki Bakari Mwamnyeto aliyesajiliwa Yanga na Nico Wadada wa Azam pamoja na kiungo Clatous Chama wa Simba ndio wachezaji waliotamba kwa majina yao kuwekwa katika vipengele vingi tofauti katika kuwania tuzo hizo.

Mwamnyeto yupo katika vipengele viwili tofauti, mchezaji bora na beki bora kama ilivyo kwa Wadada, wakati Chama ambaye jina lake limejitokeza kuwania tuzo ya mchezaji bora na kiungo bora.

MCHEZAJI BORA

Katika kipengele kikubwa cha mchezaji bora wa Ligi Kuu msimu wa 2019/2020, majina matatu ya wanaoiwania ni Nicolas Wadada (Azam), Cletous Chama (Simba) na Bakari Mwamnyeto (Coastal Union).

KOCHA BORA

Ile ya kocha bora inawaniwa na Sven Vandenbroeck (Simba) ambaye ameisaidia timu yake kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam, Thiery Hitimana (Namungo), licha ya timu hiyo kucheza msimu wa kwanza ligi kuu, amemaliza nafasi ya nne na amefika fainali ya ASFC huku Aristica Cioaba (Azam) akiisaidia timu kumaliza nafasi ya tatu.

BEKI BORA

Upande wa wanaowania tuzo ya Beki Bora ni Mwamnyeto (Coastal Union), David Luhende (Kagera Sugar) na Wadada (Azam).

KIUNGO BORA

Jina la Chama limejirudia katika vipengele tofauti na nafasi ya kiungo bora anawania na Lucas Kikoti (Namungo), pamoja na Mapinduzi Balama (Yanga)

GOLI LA KIDEO

Kipengele cha goli bora la msimu, washindani ni Sadallah Lipangile wa KMC kupitia bao lake alilofunga dhidi ya Mtibwa Sugar, Luis Miquissone (Simba), bao lake dhidi ya Alliance pamoja na Patson Shikala wa Mbeya City kupitia bao lake dhidi ya JKT Tanzania.

CHIPUKIZI BORA

Wanaowania tuzo ya mchezaji bora chipukizi ni Kelvin Kijiri (KMC), Dickson Job (Mtibwa Sugar) na Novatus Dismas (Biashara United) wakati tuzo ya kipa bora inawaniwa na Daniel Mgore (Biashara United), Nourdine Balora (Namungo FC) na Aishi Manula (Simba).

TIMU YENYE NIDHAMU

Zinazowania kipengele hiki ni Coastal Union, Kagera Sugar na Mwadui FC

MWAMUZI BORA

Wanaowania ni Ahmed Arajiga kutoka Manyara, Ramadhan Kayoko (Dar es Salaam) na Abdallah Mwinyimkuu (Singida), huku Frank Komba (Dar es Salaam), Abdulaziz Ally (Arusha) na Hamdan Said (Mtwara) wanawania tuzo ya refa bora msaidizi.

Tuzo pekee ambayo mshindi wake ameshapatikana na haijawekwa kwenye orodha ya tuzo hizo ni ile ya Mfungaji Bora itakayoenda kwa Meddie Kagere wa Simba aliyefunga mabao 22.