Chama aishusha Yanga

Sunday September 20 2020

 

By Eliya Solomon

Dar es Salaam. Ushindi mabao 4-0 walioupata Simba dhidi ya Biashara United umewafanya wekundu hao wa msimbazi kuwashusha watani zao Yanga SC kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Katika mabao manne kiungo Clatous Chama amefunga mabao mawili na kuasisti moja na kuwa mwiba kwenye lango la wapinzani wao lililokuwa linalindwa na Daniel Mgore.

Kwa ushindi huo Simba inafikisha alama saba sawa na Yanga ila wanatofautiana kwa uwiano wa magoli ya kufunga ambapo Simba imefunga mabao saba (7) na kufungwa mawili (2) huku Yanga ikifunga matatu (3) na kufungwa moja.

Azam anaendelea kuongoza kwenye msimamo huo akishinda mechi zote tatu na kufikisha alama tisa.

Mabao mengine yamefungwa na Chris Mugalu dakika ya 85 na Meddie Kageredakika ya 52.

Kagere mfungaji bora wa msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara amefungua akaunti yake ya mabao msimu huu kwenye mchezo huo.

Advertisement

Katika mchezo Kagere alionekana kuanza kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara 2020/21.

Tangu mwishoni mwa msimu uliopita Kagere alionekana kuangushwa na mfumo huku akionekana mara kadhaa kuanza John Bocco kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

Kutokuwepo kwa Bocco hata katika orodha ya wachezaji wa akiba kumetoa nafasi kwa Kagere kuanza kwenye mchezo wa leo na kufungua akaunti hiyo ya mabao kipindi cha pili.

Kagere hakucheza kwa dakika zote tisini na badala yake, alitolewa katika kipindi cha pili na nafasi yake kuingia mfungaji wa bao la nne la Simba, Mugalu aliyevalia jezi namba saba.

Aliyeonekana kuwa mwiba kwa Biashara United katika kipindi cha kwanza, alikuwa Mzambia Clatous Chama ambaye aliwafunga mabao mawili kwa umaridadi wa aina yake.

Kikosi cha Simba SC, Aishi Manila, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein, Joash Onyango, Pascal Wawa, Gerson Fraga, Luis Miquisson, Mzamiru Yassin, Meddie Kagere, Rally Bwalya, Clatous Chama.

Biashara United, Daniel Mgore, Ally Mussa, Ramadhan Chombo, Deogratius Judika, Tariq Simba, Kelvin Friday, Mpapi Nasibu, Mustha Khamis, Lenny Vedastus, Abdulmajid Mangaro, Omary Abdallah.

Advertisement