Cecafa: Hakuna Chalenji mwaka huu

Muktasari:

Kuyumba kwa uchumi kwa vyama wanachama kimekuwa ni kikwazo kikubwa kwa mashindano ya Chalenji kufanyika kila mwaka kama kalenda ya Cecafa inavyoonyesha.

Nairobi, Kenya. Baraza la Vyama vya soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) limethibisha mashindano ya Kombe la Chalenji 2018, yaliyokuwa yaanze mwishoni mwa mwezi huu, hayatafanyika tena.

Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye amesema wameshindwa kupata nchi iliyokuwa tayari kuwa mwenyeji wa fainali hizo baada ya Kenya kujitoa.

Kenya ilipata haki za kuwa mwenyeji wa mashindano hayo baada ya kuifunga Zanzibar kwa penalti na kutwaa ubingwa huo mwaka jana.

"Kwa bahati mbaya mwaka huu hatutakuwa na mashindano ya Chalenji yanayotoa nafasi kwa timu za mataifa ya ukanda huu kushindana," alithibisha Musonye.

"Tumejaribu kutafuta nchi nyingine, lakini muda haupo upande wetu kwa sababu ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu yataanza katika hatua za awali kuanzia Novemba na hadi Desemba," alifafanua Musonye.

Agosti baraza hilo lilipata na kiwewe baada ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kutangaza kutokuwa na fedha kwa ajili ya kuwa wenyeji wa fainali hizo.

Hata hivyo, Musonye alithibisha kuwa Uganda watakuwa wenyeji wa mashindano ya Chalenji Cecafa U-20, yatakayofanyika kuanzia Desemba 15-23.

"Mashindano ya vijana msimu huu yatafanyika hivi karibuni tunategemea kupata ushindani wa kweli," alisema Musonye.