CHILUNDA: Kilichomkuta Hispania ni majanga

KUREJEA nchini kwa mshambuliaji Shaaban Idd Chilunda akitokea Hispania ambako alikuwa akicheza soka la kulipwa katika klabu ya CD Tenerife kuliacha maswali mengi kwa wadau wa soka huku vyombo vya habari vikiripoti kuwa nyota huyo alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya moyo.

Kwanini maswali yalikuwa mengi? Kwa sababu Watanzania wengi wamekuwa wakipenda kuona wachezaji wa Kibongo wakipiga hatua kwa kwenda kucheza soka la ushindani katika mataifa makubwa kama ilivyo kwa nahodha wa timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta.

Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Chilunda alifunguka sababu za yeye kurejea nchini, lakini pia alizungumza mengi kuhusu maisha yake ya soka. Unajua kuwa aliwahi kucheza ndondo na wahuni wakamfanya kitu mbaya? Basi tambaa nayo.

KILICHOMKUTA HISPANIA

Chilunda anasema maisha yake Hispania yalikuwa magumu sana lakini licha ya ugumu huo alikuwa tayari kukabiliana nayo.

Anasema ugumu huo ulikuwa katika mawasiliano, benchi zima la ufundi la CD Tenerife likiongozwa na aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Joseba Etxeberria lilikuwa likiongea Kihispania sasa ikawa ngumu kwake kuelewana naye zaidi ya kuishia kuchati.

“Nilikuwa nikiishi kwa kuchati na kocha mkuu kwa sababu hatukuwa tukielewana tukionana uso kwa uso,” anasema Chilunda.

“Alikuwa akinitumia ujumbe halafu ninautafsiri kutumia google na yeye akawa anafanya hivyo. Sasa nikiwa uwanjani huwa sina simu na hakuna kitu kizuri kama kucheza kwa maelekezo. Unakuta kocha anapenda nicheze hivi lakini nawezaje kama hatuelewani, ikabidi nitafutiwe mwalimu wa lugha ya Kihispaniola.”

“Wakati nikiendelea na masomo kibaya ni kwamba, ilibidi niwe nakatisha awamu zote ambazo nilikuwa nikiitwa timu ya Taifa. Kwanza kule wakati wa mapumziko ya kupisha mechi za timu za taifa, ligi huwa zinaendelea kwa sababu kule hakuna mchezaji wa Ligi Daraja la Kwanza anayeitwa timu ya Taifa. Wengi huitwa kutoka La Liga, sasa kitendo cha kuwa Tanzania kwa wiki tatu hadi nne nikirudi nakuta kocha mpya, yule wa mwanzo kafukuzwa,” anasema.

Katika mazingira hayo Chilunda anasema ilikuwa ikimbidi kuanza moja kwa sababu kila kocha huwa na mambo yake na wakati huo alimkuta Jose Luis Oltra naye alikuwa hajui hata Kiingereza cha kuombea maji ya kunywa.

BARCELONA WAMKUBALI

Unaweza usiamini kwa haraka haraka kabla ya kufukuzwa kwa Joseba Etxeberria ambaye alikuwa akimkubali Chilunda kutokana na machapisho kadhaa ya mahojiano yake kutoka Hispania, maskauti wa FC Barcelona walikuwa wakimtazama.

Chilunda anasimulia kisa hicho kwa kusema Ilikuwa katika mchezo wake wa tatu akiwa na CD Tenerife ambao ulikuwa dhidi ya Granada CF ambao kwa sasa wanashiriki Ligi Kuu nchini Hispania. Wakati wa mchezo huo wa Ligi Daraja la Kwanza ambayo ni maarufu kama Segunda, Chilunda aliingia dakika ya 81 kuchukua nafasi ya Iker Undabarrena.

“Tulikuwa tumetanguliwa bao moja, nilicheza vizuri sana ile gemu na nikaisaidia timu yangu kupata bao la kusawazisha, nakumbuka kesho yake ajenti wangu ambaye ni wa kule kule Hispania alinicheki na kuniambia kuwa nimeandikwa katika gazeti kuwa maskauti wa Barcelona wananifuatilia kama nikiendelea kupata nafasi ya kuonyesha kiwango kizuri wanaweza kunichukua.

“Wao waliniona kama mrithi wa Suarez kwa miaka ya baadaye walitaka nipitie katika akademi yao. Nilifurahi sana lakini ndio ulikuwa mchezo wangu wa mwisho kwa sababu niliporudi nyumbani kuichezea Taifa Stars, yule kocha sikumkuta, nikakuta wamesajili na washambuliaji wengine maana timu ilikuwa katika presha ya kushuka daraja,” anasema.

ATOLEWA KWA MKOPO

Hapakuwa na namna nyingine Chilunda anasema ilibidi wamtoe kwa mkopo kwa sababu Jose Luis Oltra naye alikuwa akiongea Kihispania ndipo alipotua CD Izarra ambayo ilikuwa ikishiriki Ligi Daraja la Pili.

“Viongozi wa Tenerife walipenda niende huko kwa mkopo, hawakutaka kabisa nitoke nje ya Hispania kwa sababu nilikuwa na ofa Sweden. Mambo yalikuwa magumu zaidi katika daraja hilo la chini. Soka lao na aina yangu ya uchezaji vilikuwa vitu viwili tofauti hata kocha wao alisema kuwa sikustahili kujiunga nao.

“Soka la Daraja la Pili nchini Hispania mpira hautembei chini ni juu juu tu. Nilishindwa kuendana nao kabisa na hata ile nafasi ya kwenda Barcelona nikawa nimeipoteza. Kama yule kocha wa mwanzo angeendelea kuwa Tenerife pengine leo yangekuwa yanazungumzwa mengine,” anasema.

ISHU YA KUUMWA MOYO

Vyombo mbalimbali vya habari viliripoti kuwa Chilunda alikuwa akisumbuliwa na mtatizo ya moyo ndio maana ndoa yake na CD Tenerife ilifikia ukomo. mwenyewe anafafanua kilichotokea hadi kurejea nyumbani. “Ikumbukwe kuwa nilienda Hispania kwa mkopo.

“Sikuwa nikiumwa moyo. Tatizo nililipata lilitokana na kukaa sehemu yenye baridi sana. Kule ambako nilikuwa nikicheza kwa mkopo ulikuwa ukanda tofauti na ule ambao ipo Tenerife, mazingira yale yalinifanya niwe nasikia maumivu makali upande wa kushoto kifuani, nilipata dawa na tatizo likamalizika kabisa. Nipo fiti kwa sasa,” anasema Chilunda.

UREJEO WAKE NCHINI

Chilunda anasema hakupenda kurejea nchini lakini kwa kilichotokea ilibidi kukubaliana nacho ili ajipange upya na kupigania tena nafasi ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kama ilivyo kwa kaka zake, Simon Msuva na Mbwana Samatta.

“Kucheza nje ya nchi ni ndoto yangu, kuna mambo yanawekwa sawa, muda ukifika nitaenda sehemu nyingine kupigania ndoto zangu.” anasema.

AMVULIA KOFIA PLUIJM

Licha ya kufanya naye kazi kwa muda mfupi, mshambuliaji huyo wa Azam FC ameeleza kwamba Mholanzi, Hans van der Pluijm ni miongoni mwa makocha wake bora kabisa kuwahi kufundisha soka nchini.

Chilunda anasema alikuwa akimfuatilia kocha huyo tangu akiwa Yanga. “Binafsi nilikuwa nikipenda vile ambavyo Yanga ilivyokuwa ikicheza mpira wa chini hata alivyoenda Singida United hapakuwa na mabadiliko katika soka lake.”

“Niliona ni bonge la kocha kwa sababu sio kazi nyepesi timu ndogo kufanya ambayo waliyafanya ndani ya muda mfupi, nadhani watu wanaikumbuka ile Singida yake, walikuwa wakicheza soka la kuvutia,” anasema Chilunda.

Aliendelea kumzungumzia kwa kusema alifurahishwa mno na taarifa za kujiunga kwake na Azam baada ya kufanya vizuri akiwa na Singida United, “Niliona kuwa naweza kufanya makubwa chini yake,” anasema.

ALIVYOMUAGA

Chilunda ambaye aliondoka nchini Agosti, 2018 na kwenda kwa mkopo CD Tenerife, kilikuwa kipindi ambacho Pluijm ndio kwanza anakisuka kikosi hicho ambacho kilitwaa Kombe la Kagame baada ya kuifunga Simba mabao 2-1 katika mchezo wa fainali, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa.

“Niliondoka vizuri. Nakumbuka katika fainali nilifunga, niliacha rekodi ya kufunga mabao manane. Hakuna mshambuliaji aliyewahi kufanya hivyo. Baadaye nilisikitika kusikia ameondolewa, lakini ndio maisha ya mpira yalivyo,” anasema.

Mbali na Pluijm, Chilunda alisema wapo makocha wengi ambao anawakubali akiwemo, Etienne Ndayiragije ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya Taifa la Tanzania ‘Taifa Stars’.

Pluijm aliwahi kuweka wazi kuwa Chilunda ndiye mshambuliaji hatari zaidi wa Kitanzani kuwahi kufanya naye kazi nchini kutokana na ubunifu alionao tofauti na washambuliaji wengine ambao ni wazuri kusimama mbele tu.

BOCCO, TCHECHE WALIMPA MZUKA

Chilunda ambaye alianzia maisha yake ya soka katika Akademi ya Azam FC, anasimulia vile ambavyo alikuwa akivutiwa na safu ya ushambuliaji ya Azam FC iliyokuwa na John Bocco pamoja na Muivory Coast, Kipre Tcheche.

“Nilikuwa nikitamani siku moja kuwa kama wao, maisha yangu ikiwa mdogo ilikuwa ni kuamka na kufanya mazoezi, nilikuwa nikishinda Gym kwa sababu nilikuwa na malengo makubwa mbele yangu, nilijifunza mengi kwao maana nilikuwa napata nafasi ya kufanya nao mazoezi.

“Haikuwa rahisi muda wangu ulipofika nikaanza safari rasmi ya kucheza kikosi cha kwanza,” anasema.

AMTAKA BOCCO

Licha ya kwamba Bocco ambaye kwa sasa anacheza Simba, alikuwa ni miongoni mwa washambuliaji ambao Chilunda alikuwa akivutiwa nao kipindi anachipukia, anasema anatamani kupata nafasi ya kucheza naye kwa mara nyingine tena kikosi kimoja.

“Huwa nacheza naye timu ya Taifa na sio tatizo kucheza naye klabu moja kama itatokea,” anasema Chilunda ambaye wakati anarejea kutoka Hispania alikuwa akihusishwa kutua Simba.

SIMBA, YANGA

Chilunda anasema ni suala la muda tu kuna siku Azam itakuwa ikizunguzwa zaidi kuliko Simba na Yanga.

“Haiwezi kuwa rahisi kuangusha utawala wa Simba na Yanga. Ni jambo ambalo linahitaji muda lakini ni imani yangu kuwa ipo siku.”

Mshambuliaji huyo ambaye alifunga bao muhimu kwa timu yake katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbao FC, anasema kile ambacho kilitokea mwaka 2014 ambapo walitwaa ubingwa wa ligi ni ishara tosha kuwa inawezekana.

“achoweza kusema ni kwamba watu washike maneno yangu, Azam inaweza kuangusha utawala wa Simba na Yanga,” alisema.

TUJIKUMBUSHE KIDOGO

Tangu 2014 ambapo Azam ilitwaa ubingwa wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara hakuna klabu nyingine iliyotwaa ubingwa huo zaidi ya Simba na Yanga ambao wamekuwa wakipokezana.

Ukiiondoa Azam katika miaka hii ya elfu mbili ni Mtibwa Sugar ambao walionyesha uthubutu mbele ya wakongwe hao kwa

kuchukua ubingwa wa Ligi mwaka 2000, ambapo ilikuwa mara yao ya pili baada ya kuchukua 1999 kwa mara yao ya kwanza.

HAT TRICK YA KWANZA

Mei 20,2018 Chilunda alifunga mabao yake matatu ‘hat trick’ kwa mara ya kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao Azam iliibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wao wa nyumbani Azam Complex.

Chilunda alifunga mabao yote hayo katika kipindi cha kwanza huku kiungo Frank Raymond Domayo akifunga bao lingine kipindi hicho, kabla ya Mohammed Rashid kuifungia Tanzania Prisons la kufutia machozi kipindi cha pili.

“Ulikuwa mchezo mgumu kwa sababu Prisons walikuwa wanacheza kwa kufunga njia. Tulijitahidi kuwalazimisha kufunguka, walipokubali tu tulitumia nafasi hiyo kufunga mabao ya haraka, nilifurahia kufunga mabao matatu kwa mara ya kwanza kwenye ligi,” anasema.

NDONDO ZILIMPONZA

Wachezaji wengi wa Kitanzania kucheza mpira wa mitaani maarufu kama Ndondo ni mambo ya kawaida, Chilunda anakisa ambacho kamwe hawezi kukisahau katika maisha yake ya soka baada ya kuwafunga wahuni huko mkoani Mtwara.

“Nilikuwa kikosi B cha Azam wakati huo, nilirudi nyumbani Mtwara kwa mapumziko, kule nina marafiki zangu ambao wanacheza soka mtaani, kulikuwa na mashindano, walinipa kitu kama laki, nikaona ngoja nikacheze.

“Wale jamaa niliwafunga, sasa ile nataka kurudi nyumbani baada ya mechi, nilishangaa nachanwa na kiwembe, nilihisi ubaridi maeneo ya kifuani, nilishindwa kuwaeleza nyumbani kwa sababu mama alikuwa akiumwa ningesababisha mshtuko kwake.

“Nilijipeleka hospitali kwa kujikaza nikashonwa nyuzi karibu tisa, tangu hapo nimekuwa muoga na ndondo,” anasema.

MAISHA YA NDOA

Machi 28, mwaka huu, Chilunda ilifunga ndoa na mpenzi wake wa muda mrefu, Bi Shammy, ambaye ni ndugu wa mke wa msanii wa Bongofleva, Tundaman.

“Maisha ndani ya ndoa ni mazuri, kwa sasa nawaza kuhusu familia yangu na sio binafsi tena kama ambavyo ilikuwa zamani. Ndoa inaweza kuwa chanzo cha mambo ya mtu kunyooka,” anasema.

Chilunda alifunga ndoa hiyo pasipo kualika watu wakati wa mlipuko corona.