Bwalya ndani, Simba Tutawakeraa!

Sunday September 20 2020

 

By CHARLES ABEL

LARRY Bwalya atakuwa sehemu ya kikosi cha Simba kitakachocheza mechi ya kwanza ya ligi kwenye uwanja wa nyumbani dhidi ya Biashara United leo saa 1 usiku. Simba imetamba kwenye mitandao ya kijamii kwamba leo imepania kuwakera wapinzani wao kwelikweli.

Bwalya huenda akaanza katika kikosi cha kwanza kuchukua nafasi ya Mzamiru Yassin kama mbinu ya kusaka idadi kubwa ya mabao na kuamsha mzuka wa mashabiki wake.

Mzambia huyo tangu amejiunga na Simba akitokea Power Dynamos ya Zambia, hajacheza mchezo wowote wa ligi japo ule wa Ngao ya Jamii alikua kwenye kikosi na michezo yote hiyo Simba imecheza katika viwanja vya mikoani.

Kiungo huyo aliyeng’aa katika mchezo wa kilele cha tamasha la Simba Day, ambayo Simba ilicheza dhidi ya Vital’O ya Burundi na kuibuka na ushindi wa mabao 6-0, anaonekana kuwa katika nafasi kubwa ya kuanza katika kikosi cha kwanza leo, mbele ya Mzamiru ambaye ndiye amekuwa akitumika tangu msimu huu ulipoanza.

Dalili za Bwalya kuanza zimejionyesha katika mazoezi ya timu hiyo kujiandaa na mechi ya leo ambapo amekuwa akipangwa katika kikosi kinachoonekana ndicho kitaanza huku, Yassin akipangwa katika kile kinachoanzia benchi.

Ukiondoa Bwalya, nyota wengine wanaoonekana wana nafasi kubwa ya kuwa katika kikosi cha kwanza ni beki wa kushoto, Gadiel Michael, beki wa kati Pascal Wawa na kiungo Gerson Fraga ambao hawakuanza katika michezo iliyopita ya ugenini ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu na ule iliyotoka sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar.

Advertisement

Kikosi hicho ambacho huenda kikaanza katika mchezo wa leo kwa jinsi kilivyopangwa mazoezini kinawajumuisha Aishi Manula, Shomary Kapombe, Gadiel Michael, Wawa, Joash Onyango, Fraga, Hassan Dilunga, Bwalya, John Bocco, Clatous Chama na Bernard Morrison.

Uwezo wa kupiga pasi za mwisho kwenda kwa washambuliaji ambao Bwalya anao ukichagizwa na ubora wa eneo la kuchezea la Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao utatumika kwa mchezo huo unaonekana kwa kiasi kikubwa kulishawishi benchi la Simba kumuanzisha kiungo huyo mbele ya Mzamiru ambaye amenufaika na uamuzi wa kutomtumia Bwalya katika viwanja vya mikoani ambavyo amekuwa na uzoefu.

Kauli ya kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck kuelekea mchezo huo inaweza kuwa uthibitisho tosha wa hilo.

“Ni faida kwetu kwa sababu tunaenda katika Uwanja wa Mkapa ambao unaturuhusu kuchezea mpira ambayo ndio staili yetu na pia kuonyesha ufundi kwa hiyo tumejiandaa kwa kufanya mazoezi katika uwanja wenye nyasi za kawaida.

Aina ya mazoezi tuliyocheza ni yale ya kuhakikisha mpira unakimbia kwa kasi ikiwa ni mbinu ya kucheza soka la kushambulia,” alisema Vandenbroeck.

Simba inaingia katika mechi ya leo ikiwa na takwimu bora mbele ya wageni wao ambapo katika mechi nne walizokutana kwenye Ligi Kuu, tangu Biashara United ilipopanda daraja, imeibuka na ushindi mara tatu huku wakitoka sare mara moja.

Katika mechi hizo nne, Simba imefunga mabao nane (8) na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili tu.

Hata hivyo Simba hawapaswi kubweteka na takwimu hizo nzuri walizonazo kwani Biashara United wanaingia katika mchezo huo wakiwa na wametoka kufanya vizuri katika mechi zao mbili za kwanza ambazo wameibuka na ushindi wa bao 1-0 katika kila mchezo dhidi ya timu za Gwambina na Mwadui.

Silaha kubwa ambayo imekuwa ikiibeba Biashara United ni safu yake ya ulinzi ambayo imekuwa ngumu kufungika, ikiendeleza kile ilichokifanya msimu uliopita ambao ilimaliza ikiwa imecheza jumla ya mechi 17 bila kuruhusu nyavu zao kutikiswa na msimu huu hawajaruhusu bao lolote katika mechi zao mbili za mwanzo.

Uimara huo wa safu ya ulinzi ya Biashara United, umewafanya nyota wa Simba kujipanga vilivyo ili waweze kumaliza ubabe wao wa kutoruhusu bao kama ilivyothibitishwa na Clatous Chama.

“Msimu ndio kwanza umeanza kwa hiyo tunahitaji kuwa na rekodi nzuri haswa kwenye Uwanja wetu wa nyumbani. Tunatakiwa kuwa tunashinda kuanzia mabao mawili hadi matatu kwa kila mechi.

Tutaifanyia kazi sana na nina uhakika tutapata matokeo mazuri kwenye mchezo huu. Tunafahamu kwamba Biashara wana rekodi nzuri ya safu ya ulinzi, mechi itakuwa ngumu lakini tunajua nini cha kufanya,” alisema Chama.

Kocha wa Biashara United, Mike Baraza alisema kuwa wanaingia katika mchezo huo wakiwa na tahadhali kubwa dhidi ya Simba.

“Nimewafuatilia Sima katika mechi zao mbili za mwanzo. Hawakuanza vizuri sana lakini mwisho wa siku Simba inabakia kuwa Simba. Ni timu kubwa, ni bingwa mtetezi lakini pia watakuwa katika uwanja wa nyumbani hivyo ni lazima tuwaheshimu.

Nguvu yao kubwa ipo katika safu ya kiungo lakini sisi tunajipanga kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” alisema Baraza.

Ni timu inayoshambulia kwa pamoja na kulinda pamoja hivyo kupambana na timu kama hiyo lazima ujipange, hivyo lazima nifanye kitu katika timu kuhakikisha tunawadhibiti kwani tunataka tuendeleze moto wetu wa kuvuna pointi kila mchezo,”aliongeza Baraza.

Kabla ya mechi hiyo ya Simba, Azam FC itacheza na Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine huku ikimkosa nahodha wake Aggrey Morris ambaye ni majeruhi.

Kocha msaidizi wa Azam, Vivier Bahati alisema timu yake imejiandaa vizuri kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa saa 8 mchana.

“Tunaelewa mechi zitakuwa ngumu na ndio maana tunaendelea kujiandaa. Mbeya City wamepoteza mechi mbili hivyo hawatakuwa tayari kupoteza tena dhidi yetu kama ilivyo kwa Prisons. Tunafahamu viwanja vya ugenini vilivyo na ndio maana tumefanya mazoezi ya mwisho katika uwanja ambao unaendana mazingira. Huko Tanga, Coastal Union itawakaribisha Dodoma Jiji FC pale Mkwakwani.

Advertisement