Bruno awatia presha mastaa Leicester City

Muktasari:

Hata hivyo, ubora wa kikosi cha Ole Gunnar Solskjaer, ambacho leo kinakutana na Aston Villa, kimezidi kuwa tishio kwa Leicester kwenye mbio za kuwania kumaliza ndani ya nafasi nne za juu ili kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Leicester, England. Wachezaji wa Leicester City wamesema kiungo mpya wa Manchester United, Bruno Fernandes ni kikwazo kwao kwani, anafunga anavyotaka na hilo linawatia hofu kwenye mbio za kufukuzia tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Leicester City ambao juzi usiku walilazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Arsenal kwenye dimba la Emirates jijini London, kwa wanashika nafasi ya nne baada ya Chelsea kuichapa Crystal Palace kwa mabao 3-2 kwenye mchezo mkali wa juzi usiku.

Mabao ya Olivier Giroud, Christian Pullisic na Tammy Abraham yalitosha kuivusha Chelsea hadi nafasi ya tatu na kuacha presha kubwa kwa Manchester United inayoshika nafasi ya tano na Leicester City iliyopo nafasi ya nne kwenye kuwania tiketi ya Ligi ya Mabingwa.

Hata hivyo, ubora wa kikosi cha Ole Gunnar Solskjaer, ambacho leo kinakutana na Aston Villa, kimezidi kuwa tishio kwa Leicester kwenye mbio za kuwania kumaliza ndani ya nafasi nne za juu ili kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hapo ndipo wachezaji wa Leicester City wameanza kuihofia Man United, ambayo watakutana nayo kwenye mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu England huku Bruno akionekana tishio zaidi kwenye jeshi la Solskjaer.

Mshambuliaji wa wababe hao wa King Power, Kelechi Iheanacho alisema kasi ya Bruno na aina ya magoli anayofunga ni jambo la kuangaliwa kwa umakini mkubwa.

Kiungo Wilfried Ndidi alirekodi mazungumzo ya Mnigeria mwenzake, Iheanacho na kuyaposti kwenye mtandao wa kijamii na mazungumzo hayo yalikuwa hivi.

“Mara ngapi Greenwood amefunga?” aliuliza Ndidi, ambapo Iheanacho alijibu: “Mbili.”

Straika huyo wa zamani wa Manchester City kisha alisema: “Rashford, Martial... Bruno Fernandes kila siku anafunga. Anafunga tu siku zote.”

Mpaka sasa Bruno amefunga mabao sita na kutoa pasi za mabao tano na hilo limekuwa gumzo.