Bruno: Tunakuja kuwaziba midomo

Manchester, England. Bruno Fernandes amesema tena kwa msisitizo kwamba Manchester United itawaziba tu midomo watu wanaoochonga dhidi yao kwa kupiga mabao makali na kushinda mechi.

Na baada ya ushindi wa mabao 4-1 ugenini kwa Newcastle United, kocha wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer alisema “msimu ndo umeanzia hapa”.

Man United iliingia kwenye mchezo huo ikiwa na machungu ya kuchapwa 6-1 na Tottenham Hotspur kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu England na wengi walikuwa wakisubiri kuona kama Newcastle United ingeongeza maumivu zaidi kwa kocha Solskjaer kabla ya kwenda kuwakabili PSG kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya leo Jumanne. Mchezo huo wa St James’ Park, Juan Mata alionyesha kiwango bora kabisa na kushangiliwa wakati anatoka, ambapo alipiga pasi sahihi 59 kati ya 63, huku pasi 32 zikiwa za mbele.

Man United ilipiga mashuti 28, mengi zaidi kupigwa na timu moja ya Ligi Kuu England ndani ya msimu huu, huku mashuti 14 yakilenga goli, huku Newcastle ikishukuru ubora wa kipa wao, Karl Darlow.

Kiungo Fernandes alisema: “Timu imeonyesha uwezo mkubwa na ina wachezaji wakubwa. Ile kitu kama ya Spurs haitatokea tena kwa sababu sisi ni timu kubwa. Klabu hii ni bora kuliko matokeo yale. Hii ilikuwa safi sana, baada ya kipigo, tumerudi kivingine.