Bondia Mtanzania aliyemchapa Mkenya kwa KO awa gumzo

Muktasari:

  •  Ushindi huo sasa unamfanya Maya kuweka rekodi ya kushinda mara saba, sita kwa KO, kupigwa mara mbili kwa pointi na kutoka sare mara moja. 

Dar es Salaam.Bondia Mtanzania, Hamis Maya amekuwa gumzo baada ya kumchapa James Onyango wa Kenya kwa Knock Out kwenye ukumbi wa Charter, Nairobi.

Mtanzania huyo aliibuka mshindi raundi ya sita ya pambano lililokuwa la raundi nane la uzani wa Super welter.

Kabla ya kupanda ulingoni, Maya alikuwa na nusu nyota na pointi 0.278 wakati mpinzani wake alikuwa na nyota za pointi 7.795.

Maya amecheza mapambano 10 pekee kwenye ngumi alimduwaza Onyango, bondia mzoefu mwenye rekodi ya kucheza mapambano 37 na kushinda 24, kupigwa mara 11 na sare mara mbili.

Promota wa ngumi nchini, Shomari Kimabu alisema kiwango alichokionyeshwa na bondia huyo ni dalili njema kama ataendelezwa vema katika masumbwi.

Bondia Francis Miyeyusho alisema, Maya amepambana kwa kiwango cha juu ukinzingatia hilo ni pambano lake la kwanza kucheza nje ya Tanzania na ameshinda kwa Knock Out.

Bondia Francis Cheka alisema, Maya ameanza vizuri hivyo anapaswa kuendelezwa ili afike mbali kwani ameonyesha kiwango bora licha ya kuwa bado chipukizi kwenye ngumi za kulipwa.