Hoza apewa miwili Dodoma Jiji

Muktasari:
- Kiungo huyo alijiunga na Dodoma Jiji 2020 kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea Azam FC hadi sasa ameendelea kuitumikia timu hiyo akiwa mchezaji halali wa klabu hiyo baada ya kumaliza mkataba na waajiri wake wa zamani.
KIUNGO mkabaji wa Dodoma Jiji, Salmin Hoza ataendelea kusalia kwenye klabu hiyo hadi 2027 baada ya kuongeza mkataba miaka miwili.
Kiungo huyo alijiunga na Dodoma Jiji 2020 kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea Azam FC hadi sasa ameendelea kuitumikia timu hiyo akiwa mchezaji halali wa klabu hiyo baada ya kumaliza mkataba na waajiri wake wa zamani.
Chanzo cha kuaminika kutoka Dodoma Jiji, kimeliambia Mwanaspoti kuwa, wameanza mchakato wa kumalizana na wachezaji muhimu walioipambania timu kubaki Ligi Kuu na mambo yakiwa tayari kila kitu kitawekwa wazi.
“Mchakato wa usajili umeanza na kumalizana na wachezaji muhimu ambao tulikuwa nao msimu ulioisha kabla ya kuanza kuongeza nguvu mpya na ni kweli tumemuongeza mkataba Hoza.” alisema mtoa taarifa huyo.
Mtoa taarifa huyo alisema Hoza ni mchezaji ambaye amependekezwa na benchi la ufundi ili aweze kuongezwa mkataba kutokana na kiwango anachokionyesha na kuwa sehemu ya wachezaji muhimu kikosini.
Alisema taarifa itatolewa ni wachezaji gani wataongezwa huku akiweka wazi litafanyikka zoezi la kupunguza wachezaji ambao hawatakuwa sehemu ya kikosi chao.
“Hatuwezi kuendelea na kikosi kizima, kuna baadhi watatupisha ili kutoa nafasi kwa wachezaji wengine ambao kocha amewapendekeza waweze kusajiliwa dirisha kubwa tayari kwa msimu wa 2025/26.”
Dodoma Jiji imemaliza msimu huu ikiwa nafasi ya 12 baada ya kucheza mechi 30, imeshinda tisa, sare saba na vipigo 14 ikifunga mabao 31 na kuruhusu nyavu zake kutikishwa mara 49.