Bocco, Kagere sasa washindwe wao tu

Monday February 11 2019

 

By Charles Abel

KIKOSI cha Simba kinaendelea na maandalizi yao ya mwisho kabla ya kesho Jumanne kuliamsha mbele ya Al Ahly katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini huku nyuma mashabiki wa klabu hiyo wamepata furaha kubwa baada ya kusikia Waarabu wamekuja bila nyota wao wanne matata.

Msafara wa kwanza wa Al Ahly ukiwa na watu 40 ulitua alfajiri ya jana Jumapili wakitokea kwao na wengine wataingia leo Jumatatu, lakini wameipa afueni Simba baada ya mastaa wake wanne kutokuja nchini kutokana na kuwa majeruhi.

Beki mkongwe na nahodha wa Al Ahly, Ahmed Fathi na washambuliaji Walid Soliman, Walid Azaro na Marwan Mohsen wote wamekwama kusafiri na timu hiyo kutokana na kuuguza majeraha.

Nyota hao walikuwa miongoni mwa nyota saba wa Ahly, waliokosa mchezo wa kwanza ambao Simba ilicharazwa mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Borg El Arab, mjini Alexandria nchini Misri.

Mashabiki wa Simba baada ya kujulishwa Al Ahly wametua bila nyota wao hao, walilipuka kwa furaha, wakiamini kina Meddie Kagere, Emmanuel Okwi, John Bocco, Clatous Chama na nyota wengine wamerahisishiwa kazi.

Licha ya Waarabu kuwaacha wachezaji hao kwao, bado Simba ina kibarua kigumu cha kuwadhibiti nyota watano wa wapinzani wao ambao wamekuwa muhimili wa timu hiyo katika siku za hivi karibuni.

Licha ya Ahly kuwa na kikosi kipana ambacho kinaundwa na idadi kubwa ya nyota wenye uwezo mkubwa kulinganisha na Simba, mastaa hao watano ndio wanapaswa kuchungwa na kupewa ulinzi wa ziada.

Shughuli ya kwanza kwa Simba itakuwa dhidi ya winga Ramadan Sobhi anayeichezea Al Ahly kwa mkopo akitokea Huddersfield inayoshiriki Ligi Kuu ya England, pia kazi nyingine itakuwa ya kumdhibiti mchezaji ghali kuliko wote Afrika kwa sasa, Hassan El-Shahat ambaye timu hiyo ya Misri ilimnunua kwa dau la Euro 8.2 milioni (zaidi ya Shilingi 20 bilioni).

El Shahat ndiye alishiriki kwa kiasi kikubwa kuiteketeza Simba nchini Misri ambapo alipiga pasi tatu zilizozaa mabao kwenye mechi hiyo lakini pia yupo kiungo mshambuliaji Karim Nedved ambaye alifunga mabao matatu peke yake ‘Hat Trick’ kwenye mechi ya kwanza.

Ukiondoa hao watatu, pia yupo beki wa kushoto raia wa Tunisia, Ali Maaloul ambaye amekuwa chachu ya kuzalisha mabao kwa kufunga au kupiga pasi za mwisho kutokea upande wa kushoto wa Al Ahly.

Al Ahly imekuwa wakimtumia Maaloul mara kwa mara kutokana na kasi yake na uwezo wa kupiga pasi na kushambulia alionao ingawa pia kuna mshambuliaji Junior Ajayi ambaye mbali na uwezo wa kufunga, kukaa kwenye nafasi na kusumbua mabeki pia amekuwa akichezesha vyema washambuliaji wenzake.

Lakini wakati Simba ikiwa inaendelea kuwapigia hesabu Ahly hasa nyota hao watano, makocha na wadau mbalimbali wa soka wameipa Simba ujanja na mbinu kadhaa ambazo ikiwa watazifanyia kazi, watamaliza mapema shughuli ya kummaliza Mwarabu pale uwanja wa Taifa.

“Nilipata fursa ya kutazama mechi iliyopita waliyopoteza ugenini kwa mabao 5-0. Nilichokiona ni kwamba Simba hawakuwa makini pindi walipokuwa na mpira kwani walikuwa wakiupoteza kirahisi na baada ya kufanya hivyo hawakuwa wakijishughulisha kuutafuta tofauti na wenzao,” alisema Ali Bushir ‘Benitez’ anayeinoa Mbao Fc kwa sasa.

Naye mchambuzi wa soka na nahodha wa Yanga na Taifa Stars, Ally Mayay alisema maandalizi makubwa kwa Simba kuelekea mchezo huo yanatakiwa yawe ya kisaikolojia.

“Kuna kazi kubwa ambayo benchi la ufundi la Simba linapaswa kufanya ni kuwaweka sawa kisaikolojia wachezaji kwani matokeo ya mechi mbili zilizopita dhidi ya Ahly na AS Vita yanaonekana yamewavuruga.

Baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JS Saoura, Simba walijiaminisha kuwa wanalingana na timu nyingine za kundi hilo.

Pia Simba inapaswa kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu na zaidi ya 60% iwe ni kucheza kwa tahadhali huku wakishambulia kwa kushtukiza. Wanatakiwa kutambua kuwa Ahly ina wachezaji wa daraja la juu.

Aliongeza ni vyema wakatumia zaidi mfumo wa 4-4-2 ambao utawafanya wawe na mawinga ambao ndio wanamudu staili hiyo badala ya 4-3-3,” alisema Mayay.

Advertisement