Bigirimana,Kalengo wavishwa mabomu Yanga SC

Muktasari:

Mganda, Juma Balinya ‘JB’, huko Jangwani buana kapewa jezi namba 18 ambayo haikuwa na mtu msimu uliopita huku Patrick Sibomana akikabidhiwa jezi namba 9 na jana wakali hao walishuka kutesti mitambo kiaina kwa kucheza na timu ya Tanzanite Academy.

HUKO Morogoro Yanga inaendelea na mazoezi yao kimyakimya na jana Jumatatu kama hujasikia ni kwamba walimshushia mtu mabao 10-1, lakini mabosi wao wakaamua kuwabebesha mzigo nyota wao wapya baada ya kuwapa jezi zenye madeni makubwa.

Mabosi hao walifanya mgawanyo flani kwa washambuliaji wao wapya, Issa Bigirimana, Maybin Kalengo na Sadney Urikhob kwa kuwapa jezi ambazo kama wasipofanya jambo la maana huenda wakajikuta kikaangoni mbele ya mashabiki wa klabu hiyo.

Ipo hivi. Yanga imemaliza mpangilio wa jezi za timu yao kwa msimu ujao na mtu wa kwanza aliyepewa jezi nzito ni Mzambia Kalengo akikabidhiwa namba 19 iliyofanya makubwa msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara.

Jezi namba 19 msimu uliopita ilivaliwa na Mkongo Heritier Makambo, aliyeuzwa Horoya ya Guinea aliyefunga mabao 17 na kuwa mfungaji bora wa klabu, huku akishika nafasi ya tatu nyuma ya Meddie Kagere wa Simba na Salim Aiyee aliyekuwa Mwadui FC.

Kazi aliyonayo Kalengo ni kutakiwa kumfunika Makambo aliyewaachia mashabiki wa Yanga staili moja ya ‘kuwajaza’ iliyokuwa ikimtambulisha msimu uliopita kuwa tayari mtu keshapigwa unapoona watu wanawakusanya na kuwajaza kwa mtindo wa kupiga viganja.

Hata hivyo, Kalengo hakucheza mchezo wa jana lakini mazoezi ya Jumamosi jioni alikuwa mwiba mkali akifunga mara mbili tena mabao ya sawasawa kabla ya kesho yake Jumapili kupata maumivu ya kifundo cha mguu.

Issa Bigirimana naye buana kaachiwa msala kwa kukabidhiwa jezi namba 10 iliyoachwa na Ibrahim Ajibu aliyetimkia chama lake la zamani, Simba, huku akiwa na kazi kubwa ya kuhakikisha anafanya makubwa kupitia jezi hiyo.

Ajibu msimu uliopita alifunga mabao sita lakini alikuwa shujaa wa pasi za mwisho 17 za mabao akiwa ndiye fundi bora wa pasi hizo zilizozalisha mabao ya Yanga.

Bigirimana atakuwa na jukumu la kuitendea haki jezi hiyo akitakiwa kuwasahaulisha mashabiki wa timu hiyo machungu ya kuondoka kwa nahodha wao huyo aliyewakimbia.

Straika Sadney Urikhob ambaye bado hajatua nchini na ujio wake umekuwa ukiwa na kesho nyingi, sasa imelezwa atatua nchini ndani ya siku mbili kuanzia leo, amepewa jezi namba 17.

Mnamibia huyo ataivaa jezi hiyo ambayo msimu uliopita ilivaliwa na Amissi Tambwe ambaye alifunga mabao manane, huku akiwa na rekodi za kusisimua ndani ya soka la Tanzania katika misimu sita ya kucheza, msimu mmoja na nusu Simba na iliyosalia Jangwani.

Mganda, Juma Balinya ‘JB’, huko Jangwani buana kapewa jezi namba 18 ambayo haikuwa na mtu msimu uliopita huku Patrick Sibomana akikabidhiwa jezi namba 9 na jana wakali hao walishuka kutesti mitambo kiaina kwa kucheza na timu ya Tanzanite Academy.

WAPIGA MTU 10-1

Mechi hiyo ilipigwa asubuhi ya jana, ikiwa mchezo wa kwanza wa kirafiki ambao Kocha Msaidizi Noel Mwandila alitaka kupima jinsi mazoezi ya stamina waliyofanya kwa wiki moja yalivyoingia na vijana wake wakamchapa mtu 10-1.

Mchezo uliopigwa pale Uwanja wa kambi ya Highland, huku winga mkongwe Mrisho Ngassa akiibuka shujaa kwa kupachika mabao matatu kuandika ‘hat trick’ dhidi ya vijana hao wa Tanzanite.

Mbali na Ngassa wengine waliotupia kambani kwenye mchezo huo walikuwa, Bigirimana, Sibomana, Balinya na Mapinduzi Balama ambao ni mastaa wapya wa timu hiyo waliofunga bao moja moja kama ilivyokuwa kwa Papy Tshishimbi, Raphael Daud na Feisal Salum ‘Fei Toto’.