Big Sam awashukia wachezaji England

Saturday July 14 2018

 

 Unamkumbuka yule kocha mwenye heshima zake nchini Uingereza, Sam Allardyce maarufu kama ‘Big Sam’, ameamua kuwatolea mbovu wachezaji wa England.

Big Sam ambaye alijiuzulu kuinoa timu hiyo mwaka 2016 kutokana na kashfa ya usajili, alisema ameumizwa na kutojitambua kwa wachezaji wa kikosi hicho hasa nahodha Harry Kane.

Kocha huyo amemnyooshea kidole Kane, akisema baada ya kusifiwa kwa kung’ara katika mechi za makundi, alivimba kichwa na kujiona ndiyo kila kitu jambo lililoigharimu timu.

Alisema kuwa, kuanzia mechi za 16 bora hadi ya nusu fainali waliyofungwa na Croatia mabao 2-1 Kane hakufanya kitu chochote cha maana na hiyo inatokana na kulewa sifa.

“Ukiangalia mchezo wa nusu fainali baada ya Kieran Trippier kufunga bao wachezaji wote walibweteka na kuona kama wamemaliza kazi, hawakujituma kabisa sikumuona Kane kusaka ushindi, nahodha hapaswi kuwa hivyo,” alisema.

Alisema katika mchezo huo Kane hakufanya yale ambayo huyafanya akiwa Tottenham na kama kiongozi alishindwa kuwahamasisha wenzake kusaka ushindi.

 

Advertisement