Biashara United waita wachezaji kambini Fasta

Friday May 22 2020
Biashara pic

KOCHA Mkuu wa Biashara United, Francis Baraza amesema baada ya kurejea kwa Ligi Kuu hataki kupoteza muda na kuwataka wachezaji kufikia Jumanne wawe kambini wote ili kuanza mazoezi ya pamoja.

Ligi Kuu na michezo mingine ilikuwa imesimama kutokana na janga la Corona, ambapo juzi Rais Magufuli alitangaza shughuli za kimichezo ziendelee ifikapo Juni Mosi mwaka huu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Baraza alisema amepokea kwa furaha kurejea kwa mashindano hayo na kuwataka wachezaji wote kuheshimu mikataba kuhakikisha ifikapo Jumanne wanakuwa kambini.

Alisema lazima kila mmoja athamini kazi yake, hivyo hakutakuwa na muda wa ziada wa kumsubiri mchezaji ambaye atachelewa kujiunga na wenzake na kwamba anahitaji mechi zilizobaki kushinda zote.

“Baadhi ya waliokuwa karibu wameanza kufika kambini na tayari nimeshawajulisha wengine wote kuhakikisha siku ya Jumanne wote wawe kwenye timu, lazima kila mtu aheshimu kazi yake na mkataba” alisema Baraza.

Kocha huyo raia wa Kenya, aliongeza kuwa baada ya wachezaji kufika kambini wote, kwanza ataanzia sehemu ya utimamu wa mwili (Fitness) kisha kugeukia maeneo mengine na kutengeneza muunganiko.

Advertisement

Alisema pamoja na changamoto ndogo ndogo zitakazojitokeza lakini anaamini kwa muda watakaopewa wa kujiandaa atakisuka upya kikosi chake na kuweza kurejea kwa ubora ule ule.

“Kwanza tungeingia Jumamosi kambini (leo) lakini kwa kuheshimu siku kuu ya Eid El Fitri, ndio maana tumeweka Jumanne, nitaanza na fitness kisha muunganiko” alisema Baraza.

 

Advertisement