Benitez awatisha Arteta, Vieira kuhusu Newcastle

Thursday July 11 2019

 

NEWCASTLE, ENGLAND. KOCHA, Rafa Benitez amewaonya Mikel Arteta na Patrick Vieira kuhusu mpango wa kwenda kukinoa kikosi cha Newcastle United.

Na sasa, beki wa zamani wa Sunderland, Steve Bruce ametajwa kwamba anapewa nafasi kubwa ya kwenda kukamatia kibarua cha kuinoa timu hiyo.

Kocha msaidizi wa Manchester City, Arteta na kocha mkuu wa Nice, Vieira waliripotiwa kuwekwa kwenye orodha ya Newcastle United ya kwenda kurithi mikoba ya Benitez, ambaye hivi karibuni ametimkia China.

Lakini, ripoti zinadai kwamba Arteta ameamua kujitoa kwenye mchakamchaka huo baada ya kuzungumza na Mhispaniola mwenzake, Benitez, ambaye amekuwa akiwakosoa watendaji wa ngazi za juu katika kikosi hicho chenye maskani yake St James’ Park.

Gwiji wa Arsenal, Vieira naye alimpigia simu kocha huyo wa zamani wa Liverpool kumuulizia mazingira ya kufanya kazi kwenye kikosi cha Newcastle na hivyo kuahirisha mpango wa kwenda kwenye timu hiyo.

Newcastle walikuwa na hesabu pia za kumchukua Roberto Martinez, lakini sasa wameamua kuachana na mpango huo kwa sababu kocha huyo wa timu ya taifa ya Ubelgiji anachokihitaji kwa sasa ni kubeba ubingwa wa Ulaya akiwa na chama lake hilo lenye mastaa kibao akiwamo Eden Hazard na Kevin De Bruyne.

Advertisement

Kwa sasa, Bruce anapewa nafasi kubwa ya kuchukua mikoba hiyo huku kwa sasa akiwa kocha wa Sheffield Wednesday, aliyojiunga nayo Februari.

Advertisement