Beki Simba atoswa Uarabuni

Muktasari:

Juuko Murshid alijiunga na Simba mwaka 2014 akitokea Victoria University ya Uganda na kabla ya hapo amewahi kuichezea Vipers.

Beki wa zamani wa kati wa Simba, Juuko Murshid amejiunga rasmi na klabu ya Express inayoshiriki Ligi Kuu ya Uganda baada ya kuvunja rasmi mkataba wake na Wydad Casablanca ya Morocco ambayo ilimnasa akitokea Simba.

 

Beki huyo aliitumikia Wydad Casablanca kwa miezi minne tu kuanzia Agosti alipojiunga nayo hadi Disemba 2019 na baada ya hapo hakuonekana uwanjani kutokana na mgogoro baina yake na timu hiyo.

 

Hata hivyo baada ya kukaa nje kwa muda wote huo bila kucheza mechi za kiushindani, uzalendo umeonekana kumshinda Murshid ambaye ameamua kurejea nyumbani kuichezea Express.

 

Kocha wa Express, Wasswa Bossa amethibitisha usajili wa Juuko kupitia tovuti ya klabu hiyo huku akiamini kuwa mchezaji huyo atakuwa na msaada mkubwa kwenye timu yake.

 

"Tuna furaha kuwa na Murshid katika timu. Uzoefu wake unazungumza na hakuna shaka juu ya hilo. Nidhamu yake itawasaidia vijana wadogo kwenye timu kuwa bora," alisema Bossa.

 

Kwa upande wake, Juuko amesema kuwa amefurahishwa na usajili huo huku akisema kuwa ndoto zake ni kuiona timu hiyo ikifanya vizuri.

 

"Kwanza nimshukuru Ofisa Mtendaji Mkuu, Isaac Mwesigwa na kocha mkuu kwa kulifanya hili litokee. nina furaha kuwa hapa.

 

Express ni klabu kubwa na hatua inazopiga zinasema zenyewe. Nina uhakika tunaenda kushinda kikombe msimu huu," alisema Murshid.

 

Akiwa na Simba, Juuko alitwaa mataji mawili ya Ligi Kuu na lingine moja la Kombe la Shirikisho la Azam huku wakifanikiwa kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Kagame.