Barcelona ya Koeman ni kupaki basi katika mechi

Wednesday September 16 2020

 

Barcelona, Hispania. Kocha mpya wa Barcelona, Ronald Koeman amekiri kwamba timu yake ya msimu ujao “itapaki basi” zaidi kuliko timu nyingine zote zilizopita huko Nou Camp.

Kocha huyo wa zamani wa Everton na Southampton amechukua mikoba ya kuinoa miamba hiyo ya Nou Camp mwezi uliopita na alishuhudia timu yake ikishinda 3-1 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Daraja la Tatu ya Tarragona . Mashabiki wa Barcelona wamekuwa na wasiwasi mkubwa na timu yao, ambapo kichapo cha mabao 8-2 kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kiliwatingisha na kumfanya hata supastaa wao, Lionel Messi kutaka kuondoka. Lakini, tatizo la Messi limeshamalizwa na supastaa huyo wa Kiargentina atabaki Nou Camp.

Alisema: “Pengine tutakuwa tofauti tutaweka mkazo kwenye kikaba zaidi kuliko ilivyo kawaida ya miaka ya nyuma. Lakini, msingi mkuu ni kupeleka mpira mbele na kutafuta nafasi. Tunachotaka kukifanya kwa sasa ni kufanyia kazi soka la nguvu na wiki mbili zinazo tutahamia kwenye ufundi zaidi.”

Kikosi cha Barcelona kilimaliza hovyo msimu uliopita, hivyo wanapambana kuhakikisha wanarudi kivingine msimu ujao na kufanya mambo huku kocha Koeman akiwekeza zaidi katika kuwatumia mastaa kama Antoine Griezmann na Philippe Coutinho, aliyekuwa kwa mkopo Bayern Munich msimu uliopita.

Kuhusu msimu mpya, Messi alisema: “Siwezi kuwa na tabia tofauti eti kwa sababu tu nilitaka kuondoka. Nitajitolea kwa uwezo wangu wote.”

Advertisement