Barca yapigwa chini ofa ya kwanza ya Neymar

Friday August 23 2019

 

BARCELONA imepigwa chini katika ofa yake ya kwanza ya kumrudisha klabuni staa wa kimataifa wa Brazil, Neymar kutoka PSG huku ikitaka kumchukua kwa mkopo msimu huu kabla ya kumnunua jumla katika dirisha kubwa lijalo la majira ya joto.

Wababe hao wa Catalunya wameweka mezani kiasi cha Pauni 137 milioni mwishoni mwa msimu huu lakini PSG ilikataa papo hapo ikidai inataka Pauni 229 milioni kwa staa huyo anayetaka kurudi Hispania.

Wakati Barcelona ikienda chini ya dau la Pauni 198 milioni ililomuuza Neymar kwenda PSG mwaka 2017, PSG inataka kumuuza staa huyo kwa faida zaidi na inatazamiwa Barcelona itarudi tena siku chache zijazo.

Neymar alishatibuana na uongozi wa PSG na kufikia kuomba kuondoka kwenye klabu hiyo. Huku Rais wa PSG akisema wamechoshwa na vituko vya staa huyo.

Barcelona ina nafasi ya wiki chache hadi kufikia Septemba 2, kuweza kumrudisha Neymar kwenye kikosi chake na inaaminika itarudi na dau jingine.

Advertisement