Bao la Samatta kwa Liverpool latikisa rekodi ya Wanyama

Wednesday November 6 2019

Bao - Samatta - Liverpool -latikisa -rekodi- Wanyama-Taifa Stars-England  -Uwanja wa Anfield-Nahodha wa timu -michezo blog-Mwanasport-MwanaspotiGazeti-MwanaspotiSoka-

 

By Eliya Solomon

Dar es Salaam. Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Mbwana Samatta 'Samagoal'  ameweka rekodi usiku wa jana nchini England  ya kuwa mchezaji wa pili kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kufunga bao kwenye Uwanja wa Anfield.

Samatta aliifunga Liverpool ya Jürgen Klopp katika dakika ya 40 akiunganisha kwa kichwa mpira wa kona katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ambao KRC Genk walipoteza kwa mabao 2-1.

Mchezo huo, ulikuwa wa pili kwa Samatta kucheza dhidi ya Liverpool katika mchezo wa kwanza uliochezwa  Ubelgiji, nahodha huyo wa Taifa Stars alipachika bao ambalo lilikataliwa na teknolojia ya VAR.

Mchezaji wa kwanza wa ukanda wa Afrika Mashariki kufunga kwenye Uwanja wa Anfield ni Victor Wanyama wa Tottenham Hotspur ambaye alifunga katika mchezo wa Ligi Kuu England msimu uliopita.

Wanyama kwa sasa amepoteza nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza cha timu hiyo, alifunga bao hilo, Februari 4, 2018, baada ya kuachia mkwaju, kufuatia kutemwa kwa mpira na Liverpool, kipa, Loris Karius.

Advertisement

Mbali na manahodha hao wa Kenya na Tanzania, naye Saido Berahino aliwahi kufunga, Anfield lakini hakuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Burundi, kipindi hicho alikuwa akilitumikia taifa la England upande wa vijana.

Berahino, aliifunga Liverpool wakiwa nyumbani, Oktoba 4, 2014 wakati huo, akiichezea  West Bromwich Albion ambao katika mchezo huo, walipoteza kwa mabao 2-1.

Tangu alipopigania mambo ya uraia na kukaa sawa kisha akaanza kuichezea, Burundi huku akiwa mchezaji wa Stoke City, hakuwahi kupata nafasi ya kucheza na majoo hao wa jiji na badala yake klabu yake ilishuka daraja.

MAMBO BADO

Wakiwa wamesaliwa na michezo miwili mbele yao. Samatta anajukumu zito mbele yake ya kuisaidia KRC Genk kuhakikisha walau wanamaliza katika nafasi ya tatu ya msimamo ya kundi leo E ili kupata nafasi ya kucheza Europa Ligi katika hatua ya 32 bora.

KRC Genk wanaburuza mkia katika kundi hilo, wakiwa na pointi moja, wanaoongoza msimamo ni Liverpool wenye pointi tisa, Napoli nane huku Salsburg wakiwa na pointi nne katika nafasi ya tatu.

Michezo miwili iliyosaliwa kwa KRC Genk ni dhidi ya Napoli utachezwa ugenini Italia na watamaliza nyumbani dhidi ya Salsburg. Timu mbili zitakazomaliza katika nafasi ya kwanza na pili katika kila kundi husonga mbele katika hatua ya mtoano.

Advertisement