Banka aipa nguvu Yanga kuimaliza Simba

Tuesday July 7 2020

 

By Khatimu Naheka

Siku chache kabla ya kuvaana na Simba kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam, Yanga imepata nguvu baada ya kurejea kundini kwa kiungo Mohamed Issah 'Banka'.

Mechi hiyo itachezwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar, Jumapili, Julai 12.

Kiungo huyo hajaichezea Yanga tangu ligi iliposimama Machi 17 kutokana na agizo la serikali la kusimamisha shughuli za michezo kama njia za kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona.

Banka ameungana na kambi ya timu hiyo leo asubuhi na baada ya hapo akawa miongoni mwa wachezaji waliohudhuria mazoezi ya mwisho leo jioni kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera kabla hawajaivaa Kagera Sugar kesho.

Kitendo cha Yanga kuhakikisha kiungo huyo anaungana na wenzake haraka ni wazi kwamba kinaashiria inautazama zaidi mchezo dhidi ya Simba ambao umeshikilia tiketi yao pekee iliyobakia ya kuwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa msimu ujao.

Yanga imejikuta ikikabiliwa na mzimu wa majeruhi baada ya baadhi ya wachezaji wake tegemeo kupata majeraha siku chache kabla ya kuwavaa Simba.

Advertisement

Hadi sasa timu hiyo inawakosa Mapinduzi Balama aliyevunjika mguu lakini pia inamkosa nahodha Papy Tshishimbi ambaye anasumbuliwa na majeraha ya goti.

Kana kwamba haitoshi, kiungo Haruna Niyonzima yupo kwenye hatihati ya kucheza mechi dhidi ya Simba baada ya kuumia kwenye mchezo dhidi ya Biashara United.

Advertisement