Bandari yamkazia maisha Shikalo

Thursday July 4 2019

 

By Thomas Matiko

Nairobi. Klabu ya Bandari FC imemkazia maisha kipa Faraouk Shikalo kwa kusisitiza kuwa bado ni mchezaji wao licha ya mlinda lango huyo kuripotiwa kutia saini mkataba wa kujiunga na Yanga ya Tanzania.

Shikalo mwenyewe alithibitisha kufanya maongezi na viongozi wa Yanga na hata kutia sahihi mkataba wa kujiunga nao ikiwa ni baada yao kumfuata huko Cairo Misri kuhakikisha wanakamalisha usajili wake.

“Ni kweli hatimaye nimesaini nao na nafurahia uhamisho huu nikiwa mwingi wa matumaini kuwa huko niendako pia nitaweza kutia fora” alinukuliwa Shikalo akiwa Misri siku tatu zilizopita

Hata hivyo kulingana na afisa mkuu mtendaji wa Bandari, Edward Oduor, klabu hizo mbili zipo kwenye harakati za majadiliano ila  bado hawajaafikiana kuhusu uhamisho wake.

“Yeye bado ni mchezajio wetu. Bado angali ana miezi sita kwenye mkataba wake nasi. Hatujamwachia bado na wala hatuna mpango wa kumzuia kama anataka kuondoka. Kwa upande wetu, tuna mpango wa kufanya mazungumzo na Yanga Jumamosi hii” Oduor kaeleza.

Yanga wamekuwa wakimwindwa Shikalo kwa kipindi cha miezi sita sasa toka walipoucheki uwezo wake kwenye dimba la Sportpesa Cup lililoandaliwa kule Dar es Salaam Tanzania Januari mwaka huu Bandari ilipoishia kufika fainalini.

Advertisement

Hata zaidi waliendelea kumfuatilia ligini ambapo alisajili takwimu za kuridhisha mno.  Msimu uliopita, kipa huyo alihusika kwenye mechi zote za Bandari ligini isipokuwa ya mwisho dhidi ya Nzoia Sugar, mchango wake ukiwasaidia kumaliza katika nafasi ya pili kwenye ligi.

Vile vile alikuwa langoni kwenye fainali ya dimba la GOTV Shield Cup na kuisaidia timu kubeba ubingwa kwa kuwalima Kariobangi Sharks.

Kwenye ligi, Shikalo alifanikiwa kumaliza kwa kutofungwa kwenye mechi 12 huku akiruhusu magoli 29 pekee.

Advertisement