Bandari wawaonya kwa Al Ahli Shandy

Thursday August 22 2019

 

By Abdulrahman Sheriff

Mombasa. WACHEZAJI wa Bandari FC wameapa kuhakikisha hawacheki hapo kesho wakati watakapojitupa uwanjani huko Sudan kupambana na Al Ahli Shandy kwenye mechi ya marudiano ya raudi ya kwanza ya Caf Confederation Cup.

Baadhi ya wachezaji waliohojiwa na Mwanaspoti kabla ya kuondoka nchini kwenda huko Sudan ambao hawakutaka kutajwa majina, walisema kesho siku ya Ijumaa hawataki mzaha kabisa ila kucheza kufa kupona kuhakikisha wanarudi nyumbani na ushindi.

“Hatuendi Sudan kwa sababu ya kukamilisha ratiba yetu bali tunaelekea huko kuhakikisha tunawapa mashabiki wetu na Wakenya ushindi.

“Ndipo nasema tunasafiri kwenda kukutana na Shandy tukiwa hatutaki mzaha aina yoyote isipokuwa kufunga magoli,” alisema mchezaji mmoja.

Mwanasoka mwingine anayechezea nafasi ya ulinzi alisema kuwa watahakikisha hakuna mtu anawapenya na akaeleza kuamini kuwa mastraika wao watratekeleza wajaibu wa kufunga mabao na kuondoka Sudan kurudi nyumbani na ushindi.

“Tuko fit and ready for the job. Tunataka kuhakikisha tunatimiza ahadi ya kusonga mbele kwenye dimba hilo la Afrika.

Advertisement

“Tuna imani tunazidi kupata uzoefu na tunataka tuibuke washindi huko ugenini,” akasema difenda huyo.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Admiral Youth FC, Aref Baghazally aliwaomba wanasoka wa Bandari wacheze bila ya kuwa na wasiwasi wowote kwani anaamini soka la kisasa hakuna advantage yoyote kwa timu ya nyumbani lazima kupata ushindi.

“Tunachokihitaji Ijumaa ni Bandari yetu kupata ushindi. Tuna kikosi kizuri kinachoweza kuibuka washindi katika pambano hilo,” akasema Baghazally ambaye aliwataka maofisa wa timu hiyo wamfikie balozi wa Kenya aweze kuwaomba Wakenya wafike kiwanjani kuishangilia timu yao.

Advertisement