Bajeti ya Simbu si mchezo mwanangu

Muktasari:

  • Bajeti ya vifaa atakavyovitumia mwanariadha nyota nchini, Alphonce Simbu kwenye mbio za New York City marathoni za Septemba 4 si  ya mchezo kwani wadhamini wake, kampuni ya Adidas imemuandalia vifaa vyenye thamani ya Sh 198000 ambavyo ni raba na jezi kwa ajili ya mbio hizo ambazo bingwa ataondoka na kitita cha Sh 220 Milioni pale Marekani.


NYOTA wa riadha nchini, Alphonce Simbu amebakiza siku 11 tu za kuamua kubadili maisha yake moja kwa moja, endapo atashinda kwenye mbio za New York City Marathoni Novemba 4 kule Marekani.

Yote tisa, unaambiwa kwenye mbio hizo, vifaa atakavyovitumia Simbu siyo vya mchezo mchezo kwani ni pesa ya matumizi ya mwezi mzima kwa mtu anayetumia bajeti ya Sh 5,000 kwa siku na bado chenji inabaki.

Simbu mwenyewe anakwambia hata bei ya vifaa hivyo haijui, anachokijua yeye atavikuta Marekani siku chache kabla ya mbio hizo ambazo bingwa ataondoka na kitita cha Sh 220 Milioni, achilia mbali bonusi ya fedha nyingine atakayoipata kama atavunja rekodi.

Kwenye mbio hizo, Simbu anatarajiwa kuvaa raba ya adidas adizero Boston 6 ambayo kwa haraka haraka si chini ya dola 55 ingawa awali ilikuwa ikiuzwa dola 179.

Kwenye jezi, mshindi huyo wa medali ya shaba ya dunia atatupia bukta na fulana ya Adidas Response Tee ambayo si chini ya dola 35 ambavyo kwa fedha ya Tanzania, vifaa vyote ni Sh 198,000.

“Ki ukweli sijui bei ya vifaa hivyo, ninachokifahamu ni kwamba nitakapofika Marekani, Adidas wataniletea kule,” alisema Simbu.

Alisema mipango yote ya yeye kushiriki mbio hizo inafanywa na wadhamini wake, na yeye atakapowasili Marekani Novemba Mosi atakabidhiwa chipu ya kuvaa mkononi ambayo itakuwa ikirekodi kilomita na njia atakazokuwa akipita kwenye mbio hizo.

“Nimejiandaa vizuri, japo ilikuwa ndani ya muda mfupi, lakini kwa sasa niko fiti kupambana,” alisisitiza Simbu aliyewahi kutwaa medali ya dhahabu ya mbio za Mumbai marathoni na kumaliza wa tano kwenye Olimpiki iliyopita ya Rio 2015 na nafasi kama hiyo kwenye mbio za London marathoni mwaka jana.