BMT yaifungia mbio ya Kigamboni marathoni

Muktasari:

Kuanzia Januari Mosi 2020, vibali vyote vya kuendesha mbio za Marathoni na mbio nyingine za barabarani ngazi ya Taifa, mkoa na wilaya vitatolewa na Baraza na si RT.

Dar es Salaam.Baraza la Michezo la Taifa (BMT) imeifungia mbio ya Kigamboni International Marathon pamoja na kutoa maagizo kwenye Shirikisho la Riadha Tanzania (RT).

Kaimu Katibu Mkuu wa BMT, Neema Msitha amesema wameifungia mbio hiyo kutofanyika kwa mwaka mmoja.

Uamuzi huo umekuja siku moja baada ya mbio hizo kufanyika Jumapili ya Desemba Mosi huko Kigamboni nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

"Hawakufuata sheria na kanuni za uendeshaji wa mbio za Marathoni. Mwandaaji wa mbio hizo pia anatakiwa kuhakikisha anakamilisha kulipa zawadi alizotakiwa kutoa zawadi kwa washindi kabla ya Disemba 12, 2019," alisema Msitha.

Mtendaji huyo wa BMT alisema kumekuwa na changamoto katika mbio za marathoni nchini ikiwa baadhi ya waandaji kutosajiliwa.

"Kuna mbio kunakosekana ulinzi barabarani, huduma za afya, maji katika vituo na waandaaji kushindwa kutoa zawadi kwa mabingwa jambo linalosababisha mgogoro kati ya wandaaji, washiriki na wadau.

Alisema kuanzia Januari Mosi 2020, vibali vyote vya kuendesha mbio za Marathoni na mbio nyingine za barabarani ngazi ya Taifa, mkoa na wilaya vitatolewa na Baraza na si RT.

Aidha BMT limezielekeza mamlaka za usimamizi wa Michezo ngazi ya Mikoa na Wilaya kuhakikisha kuwa hamna mbio yoyote ya barabarani inafanyika bila kibali cha Baraza la Michezo la Taifa.

Kwa mujibu wa Sheria ya BMT waandaji wote wa mbio hizo wanapaswa kulipia asilimia moja ya tiketi au viingilio vya mbio, kwenda katika mfuko wa maendeleo ya Michezo BMT.

Akizungumzia tamko hilo, makamu wa pili wa rais RT ufundi, Dk Hamad Ndee alisema usajili wa mbio ndiyo utafanyika BMT na RT itaendelea kusimamia.

"Zamani ndiyo ilivyo kwenye usajili tu na kusimamia ni jukumu letu, ila maamuzi rasmi ya RT yatatolewa baada ya kikao cha kamati ya utendaji," alisema.