BARBARA: Hao Yanga waleteni hata leo

KATIKA mfululizo wa makala ya Mtendaji Mkuu mpya wa klabu ya Simba, Barbara Gonzalez jana alianika mikakati yake ya kutaka kuifanya klabu hiyo kuwa kama Zamalek ya Misri ama klabu nyingine za Afrika Kaskazini katika kujiendesha kwa faida na kufanya usajili wa maana.

Leo katika muendeleo huo, Barbara anaanika kiu yake ya kutaka kupunguza gharama za uendeshaji na pia kuzungungumzia usajili wa Yanga na Azam na chagamoto ambazo anahisi watakumbana nazo kutoka kwa wapinzani wao hao katika Ligi Kuu Bara. Pia anakiri Yanga imefanya usajili mzuri na msimu huu inaonekana kama imepania kurejesha mataji, ila kwa aina ya kikosi alichonacho Msimbazi, anatamani hata leo wakutane ili wawanyooshe tena. Endelea naye...!

PANGA GHARAMA ZA UENDESHAJI

Simba inakadiriwa kutumia kiasi cha Sh 5 Bilioni kwa mwaka ikiwa ni pamoja na fedha za usajili, mishahara na gharama nyingine za uendeshaji wa klabu hiyo.

Jambo hilo kwa Barbara amelifafanua na kusema mbali na mipango yake ya kuongeza kipato cha klabu, lakini mkakati wake mkubwa ni kupunguza gharama katika shughuli mbalimbali za uendeshaji wa timu, ili kuhakikisha Simba inapata faida kubwa zaidi na kufikia malengo yao.

Anasema gharama hizo zipo katika maeneo mengi ambayo kwa sasa wanayafanyia kazi na kufafanua;

“Kwa mfano, badala ya kununua maji ya rejareja kwa ajili ya matumizi ya wachezaji na makocha, tutakuwa tunanunua maji kwa bei ya jumla, huu ni mfano wa kawaida sana.”

Anasema pia timu pia inaweza kupunguza gharama za usajili kwa kutengeneza mfumo mzuri zaidi wa kuzalisha na kuimarisha timu za vijana ili kipindi cha usajili waepuke kununua wachezaji wa gharama kubwa.

“Klabu yoyote lazima iendeshwe kwa malengo ya kutengeneza faida na moja ya sehemu ya kuhakikisha tunapunguza gharama kubwa ni ishu za usajili kwa ajili ya kuimarisha kikosi.

TUNAFUNGWAJE NA YANGA

Licha ya kutokuwa na muda hata wa miaka mitano katika masuala ya soka, Barbara anasema kamwe hatishiki na watani wao wa jadi, Yanga katika Ligi Kuu Bara.

Barbara anasema anajua upinzani mkubwa wenye kila aina ya majigambo baina ya timu hizo mbili, ila anasema Simba bado ni bora sana katika Ligi na hata mashindano mengine kama Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Anasema anaamini ushindani upo baina ya timu hizo, ila si kwa kiwango kikubwa na anajivunia kipigo cha mabao 4-1 walichoipa Vijana wa Jangwani kwenye michuano ya Kombe la FA (ASFC)

“Naweza kuonekana tofauti, lakini Simba ya sasa ni tofauti na ya miaka ya nyuma, kwani tumewekeza katika timu na benchi la ufundi. Hii pekee inatupa jeuri ,” anasema Barbara na kuongeza;

“Katika ligi, Yanga ilisawazisha mabao mawili na katika mechi ya marudiano Simba ilipoteza kwa bao 1-0. Hata hivyo tulijiuliza na kuwafumua kwenye Kombe la Shirikisho. Msaada mkubwa unaotolewa na Mohammed Dewji ‘Mo’ , kambi ya kisasa, mishahara inalipwa kwa wakati na bonasi ya mechi unafungwaje na Yanga?”

Anasema kuna sehemu walipotea na kuamua kurejea kwani kuna usemi unasema kuwa mtu anapotea njia wakati wa kwenda tu, si wakati wa kurudi,” alisema Barbara.

Kwa mujibu wa Barabara, waliamua waliweka mikakati ya kulipiza kisasi pamoja na kuwa mechi haikuwa ya Ligi Kuu na kufanikiwa kushinda kwa mabao 4-1.

Anasema wanaheshimu uwezaji wa Yanga kupitia msimu huu, lakini watabaki kushindana tu, lakini hawatashinda.

“Tunajua Yanga ndio timu pinzani na mtani wa jadi wa Simba, hilo halina ubishi, lakini kwa sasa tumewaacha mbali, Simba imepiga hatua katika masuala mengi na mengine yanasubiri utekelezaji tu, tunaheshimu uwepo wa Yanga, lakini si kwa ushindani nasi,” anasema.

USAJILI WA YANGA ANAUONAJE?

Yanga kwenye dirisha la usajili lililofungwa mwezi uliopita, imesajili wachezaji wapya 12 wakiwamo watano wa kigeni na wazawa saba na mitaani mashabiki wao wamekuwa wakitamba kwamba wataikomesha Simba kwani kikosi chao kimeimarika kwelikweli.

Hata hivyo, Barbara anapoulizwa juu ya usajili huo anakiri ni kweli kwa msimu huu, watani wao wamejitahidi kuongeza nguvu, ila Simba nayo haikubaki nyuma na kuongeza nguvu ili kuendeleza wimbi la ushindi.

“Kwa sasa, Yanga imebaki kutupa changamoto na kutustua sisi kuwa kuna upinzani, ila sio kama ule wa miaka ya nyuma. Kwa kifupi, upinzani uliopo sasa ndio chachu ya maendeleo ya timu yetu na naamini itatupa taswira halisi wapi tunaenda kwa sasa,” anasema.

Anasema kuwa yeye anapenda ushindani katika kila sekta ili kuleta tija katika fani usika.

“Simba kwa sasa imeshinda mataji matatu katika Ligi Kuu Bara. Tunahitaji changamoto mpya na wala si vinginevyo,” anasema Barbara na kufafanua kuwa mpango mkakati uliopo sasa ni kuhakikisha timu infanya vizuri katika mashindano ya ndani na ya kimataifa.

“Kuna Ligi ya mabingwa Afrika, ni mashindano makubwa sana, bado tunasotea matokeo ili tuweze kutimiza ndoto yetu pamoja na changamoto zilizopo sasa,”

Anafafanua usajili wa msimu huu wa Ligi kwa Yanga na Azam umewafanya wao kufanyakazi muda wote ili kuhakikisha kuwa wanasimama kwenye mistari ili kuhakikisha wanawafunika zaidi.

“Yanga imesajili wachezaji wazuri ambao tunaamini italeta ushindani katika ligi, tunajua wanataka kurejesha mataji yaliyohamia Msimbazi, ila niseme wazi hakuna timu itakayoweza kufikia mafanikio yetu,” anasema Barbara kwa kujiamini.

Kuhusu upande wa Azam FC, Barbara anasema kuwa ni moja ya timu nzuri na imefanya usajili kwa umakini mkubwa.

Anasema wanatarajia kupata ushidani mkubwa sana na hasa baada ya timu hiyo kusajili wachezaji wenye ushindani.

“Yanga na Azam nazo zinataka kutwaa ubingwa kama sisi, labda miaka mitano au 10 ijayo, sisi tumejidhatiti sana na lengo letu ni kuwafanya wana Simba kuwa na furaha muda wote,” anasema.

Anasema kwa sasa, Yanga na Azam FC zitabikia kuwa timu zinazoleta changamoto kwao kama timu nyingine na wala si upinzani.

“Naomba niwatoe wasiwasi wanasimba, uongozi wa klabu umejipanga kuhakikisha wanafanya vyema katika kila mashindano na kuleta maumivu kwa timu nyingine.”

LIGI YA MABINGWA AFRIKA

Barbara anasema Bodi ya Wakurugenzi chini ya Mwenyekiti Mohammed ‘Mo’ Dewji inajua kazi kubwa wanayokabiliana nayo kuhusiana na mashindano hayo.

Anasema mashindano ya msimu uliopita hayakuwa mazuri kwa klabu yao na kulazimika kufanya mabadiliko ya benchi la ufundi.

“Safari hii mambo ni tofauti sana, Ligi ilipangwa kuanza Novemba mwanzoni, sasa itafanyika mwishoni mwa mwezi huo. Hii ni fursa kwetu kujipanga vizuri zaidi ili kukabiliana na mpinzani yoyote ambaye tutapangwa naye,” anasema. Kwa mujibu wa Barbara, wana mikakati ambayo ina malengo ya kuwafikisha hatua za juu kabisa katika mashindano hayo makubwa sana barani Afrika.

“Jukumu la uongozi ni kutimiza yale ambayo yanatakiwa katika kufikia malengo, kama eneo zuri la kufanyia mazoezi (uwanja), Vifaa, chakula na motisha kwa wachezaji. Hivyo vyote vinafanyika tena kwa uhakika zaidi. Hakuna mchezaji wala mfanyakazi wa Simba anaye kosa stahiki zake kwa muda muafaka.”

WITO KWA WANAWAKE

Barbara anasema wadau wengi wa soka wanashangazwa naye kwa kuwa kiongozi wa timu kubwa kama Simba akiwa na umri mdogo na tena ni mwanamke. Anasema ameshangazwa sana na maoni ya watu kuhusiana na yeye huku wengine wakiponda uteuzi wake bila kujua ni mtu wa aina gani.

“Miaka ya nyuma, mashabiki na wanachama wa klabu ya Simba walikuwa wanafikra kuwa kuwa kiongozi wa klabu kubwa lazima uwe na miaka zaidi ya 45 na kuendelea. Hali hiyo ilitokana na watu kuwa waoga wa fikra, hali ambayo kwa jamii imetawala sana. Binadamu anatakiwa kuwa na uthubutu na kufanya kile ambacho amekipanga,” alisema.

Anaongeza ukiwa muoga na kutilia maanani mambo unayosikia kuhusiana na wewe, basi hautaweza kufikia malengo uliyojiwekea.

“Leo hii, kuna watu wanafanya mambo mema, wanatoa sadaka hata kufikia dola milioni moja, lakini bado watu watakusema vizuri na wengine wanakusema vibaya. “Shida itakuja endapo utawasikia na kutilia maanani wanayosema, hapo utashindwa kufika, dawa hapa ni kuziba masikio na kuendelea na kile ulichokipanga,” anasema.

“Mimi ni kijana wa Kitanzania ninayeongoza klabu kubwa yenye idadi kubwa ya mashabiki, macho ya wana Simba yanamwangalia yeye, masikio yanasikia mambo ambayo yanatoka kwake, lazima afanye kile kitu ambacho wana Simba wanakitarajia ambacho ni matokeo mazuri katika timu na maslahi ya kila mchezaji na wafanyakazi wengine,” anasema. Anawataka vijana kutojiweka nyuma katika masuala ya uongozi kwani wao ndiyo damu changa ambayo wanategemewa kuleta chachu ya maendeleo katika klabu na sekta nyingine.

“Hakuna mzee hasiyepitia ujana, ila wao walikuwa na uthubutu wa kufanya ambayo wao (vijana) wameyaona au wanayaona, na wao pia wanahitajika kufanya mambo ambayo yataacha kumbukumbu na heshima kwa jamii,” anasema.

Pia amewataka wanawake kutokuwa nyuma na kudhani kuwa mpira wa miguu unaongozwa na wanaume tu.

“Nina furahi kuona kwenye bodi ya Simba kuna mwanamke mwingine (Asha Baraka) ambaye amejitolea kufanya kazi za klabu, hivyo wanawake wana nafasi na wanatakiwa kutumia fursa hiyo,” anasema.

Aliongeza soka kwa sasa unachezwa na wanawake pia na timu yao ya Simba imeweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na kuwataka wanawake vijana kuanza kujifunza kucheza mpira kwani ni ajira kwao.

AMTAJA MO DEWJI

Barbara anasema kufanya kazi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba, Mohammed Dewji kumempa uzoefu mkubwa sana na kumfanya ajiamini.

Anasema kuna baadhi ya kazi alizokuwa anazifanya zimekuwa na fundisho kubwa sana kwake na kujua mambo mengi.

“Dewji anafanya mambo mengi sana ya Simba mpaka kufikia hapa ilipo. Mengi anafanya kwa kujitolea kama mwanachama wa klabu ili kuona Simba inafanya vizuri, hilo limefanikiwa pamoja na ukweli kuwa mpira una matokeo matatu,” anasema.

Anafafanua kuwa jinsi Dewji anavyoisaidia Simba kwa sasa na mafanikio yaliyopatikana, yanawafanya mashabiki kuamini kuwa Simba haitafungwa wala kutoka sare na timu yoyote hapa nchini, jambo ambalo siyo kweli kwani kuna matokeo mengine ni ya ajabu sana na huwezi kuamini. Anasema katika kuhakikisha Simba inapata maendeleo kupitia mfumo wa kisasa, alimwezesha kukutana na watu wa La Liga, Bundesliga na klabu mbalimbali ili kujua uendeshaji wa klabu mbalimbali na kupata maendeleo.

“Mambo mengi ya mpira kama vile kukutana na Rais wa Fifa ilitokana na mawazo ya Dewji na haya yote yamefanyika kwa ajili ya kuleta maendeleo ndani ya Simba, ipo wazi Mo Dewji ameiwezesha Simba kufikia hapa ilipo,” anasema. Anasema Mo Dewji amepania kuiweka Simba katika chati ya juu Afrika na timu yenye mafanikio, hivyo anahitaji ushirikiano.

“Kuna mambo mengi yanafanyika ya kumkatisha tamaa, hata hivyo, mwenyewe ameweka wazi kuwa hatoondoka ndani ya klabu ya Simba, hii ni faraja kwa bodi ya wakurugenzi, wanachama, mashabiki, wachezaji na wadau wengine,” anasema.