Azam yakaa kileleni, waisubiri Dodoma Jiji

Muktasari:

Azam imeanza kujikusanyia pointi za ugenini katika mchezo wao wa kwanza nje wakiwa jijini Mbeya.

BAO la Ally Niyonzima alilofunga kwa kichwa dakika ya 25 akiunganisha kona ya Never Tigere limeifanya klabu ya Azam Fc kukaa kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Ushindi wa 1-0 unawafanya Azam Fc kufikisha pointi tisa kwenye mechi zake tatu huku wakiwa wamefunga magoli manne mpaka sasa katika msimamo wa Ligi Kuu.

Hali hiyo inawafanya wawashushe kileleni Yanga wenye pointi saba wakiwa wamecheza mechi tatu na KMC waliokuwa wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi sita wakiwa wamecheza mechi mbili tu.

Azam ni kama wamekaa kileleni kwa muda tu kwani wanawasubili mchezo wa Coastal Union dhidi ya Dodoma FC ambao kama Dodoma wakipata ushindi basi watawashusha Azam kutokana na wao kufikisha pointi tisa kwenye mechi tatu huku wakiwa hawajaruhusu bao lolote na wakiwa wamefunga magoli matatu kwenye mechi mbili.

Wakati huo huo Azam na Dodoma zikiwa zinawindana katika kukaa kileleni, kesho septemba 21 saa 8:00 mchana KMC watakuwa na kibarua kingine cha kukaa kileleni dhidi ya Mwadui Fc mchezo utakaopigwa katika uwanja wa Mwadui Complex.

KMC njia pekee ya kurudi kileleni ni kushinda mchezo huo, mpaka sasa wana pointi sita katika mechi mbili huku wakirihusu nyavu zao ziguswe mara moja.

Afisa Habari wa Azam FC, Thabit Zakaria amesema mchezo wao dhidi ya Mbeya City ulikuwa mgumu kutokana na wapinzani wao kucheza mipira ya juu lakini pia wakitumia nguvu nyingi.

"Kitu ambacho hatujakipenda ni mashabiki wa Mbeya City kutushambulia sisi kwa kuturushia mawe, sio wote wapo wale wastaarabu lakini watu wa usalama walituliza" alisema msemaji huyo anayefahamika kama Zaka.