Azam FC yaifanya Yanga ngazi

Muktasari:

  • Cheche aliielezea Lipuli kiufundi kwamba ina ushindani wa hali ya juu kuanzia safu yao ya mbele, viungo na mabeki, jambo alilodai wanajipanga vilivyo kuhakikisha wanafanikisha kutwaa ubingwa wa FA, utakaowafanya washiriki michuano ya Shirikisho la Afrika.

AZAM FC wamebakiza mechi mbili za Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar na Yanga, sasa benchi la ufundi la timu hiyo limepanga kuzitumia kama maandalizi ya kuivaa Lipuli katika fainali ya Kombe la FA Juni Mosi kwenye Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi.

Kocha wa timu hiyo, Idd Cheche alisema kutokana na ubora wa Mtibwa Sugar wanayocheza nayo leo Jumatano kwenye uwanja wao, anaamini itawapa mwanga wa kile watakachokifanya katika fainali ya FA.

Cheche aliielezea Lipuli kiufundi kwamba ina ushindani wa hali ya juu kuanzia safu yao ya mbele, viungo na mabeki, jambo alilodai wanajipanga vilivyo kuhakikisha wanafanikisha kutwaa ubingwa wa FA, utakaowafanya washiriki michuano ya Shirikisho la Afrika.

“Nafasi pekee muhimu kwetu itakayotufanya tushiriki michuano ya kimataifa ni kupambana kwa hali na mali kuwafunga Lipuli ambayo ni timu inayojua kupambana na ndiyo maana imefikia hatua hiyo.

“Itakuwa fainali ngumu hivyo tunajipima dhidi ya Mtibwa Sugar na Yanga ambayo tutacheza nayo mechi ya mwisho ya ligi, hizo zitatusaidia kugundua udhaifu na ubora wetu,” alisema.

Viongozi wa timu hiyo wapo sambamba na benchi la ufundi kuhakikisha wanatwaa taji la FA kama alivyosema mkurugenzi wa ufundi, Abdulkarim Amin ‘Popat’.