Avire apewa jukumu la kuwaua Madagascar, Olunga kuanzia benchi

Muktasari:

Eric Johanna atasimama nyuma ya Avire, wakisaidiwa na mawinga wawili, Francis Kahata atakayesimama kwenye winga ya kushoto huku Ayub Timbe, akifanya yake winga ya kulia.

KAMA alivyoahidi jana Alhamisi baada ya programu ya sita ya mazoezi ya timu ya taifa ya Kenya 'Harambee Stars', Kocha mkuu Sebastien Migne, amempumzisha straika tegemeo wa Stars, Michael Olunga dhidi ya Madagascar leo Ijumaa usiku.
Katika mchezo huo, ambao ni wa kwanza kati ya miwili ya kujipima nguvu, ambao utapigwa kuanzia saa 3 usiku, ugani Stade Robert-Robin, jijini Paris ambapo mashambulizi ya Stars yataongozwa na John Avire.
Olunga, anayekipiga klabu ya Kashiwa Reysol ya Japan, alijiunga na kambi ya Stars, iliyoko Paris jana asubuhi, kabla ya kushiriki mazoezi ya jioni, hayuko fiti kuanza lakini ataingia kipindi cha pili.
Mbali na Olunga, Stars ina mastraika wengine wawili; Masud Juma na Christopher Mbamba, ambao watalazimika kusubiri benchi katika mfumo wa 4:3:3 ambao hata hivyo kwa mujibu wa staili ya uchezaji wa Migne utawategemea zaidi mawinga.
Eric Johanna atasimama nyuma ya Avire, wakisaidiwa na mawinga wawili, Francis Kahata atakayesimama kwenye winga ya kushoto huku Ayub Timbe, akifanya yake winga ya kulia.
Nahodha Victor Wanyama na Dennis Odhiambo watacheza kama viungo wawili wakabaji. Golini atasimama mlinda lango wa St. George ya Ethiopia Patrick Matasi wakati Philemon Otieno, Abud Omar, Brian Mandela na Musa Mohammed watasimama nyuma.
Kikosi kamili:
18. Patrick Matasi (Kipa), 20. Philemon Otieno, 3. Abud Omar, 5. Brian Mandela, 2. Musa Mohammed, 12. Victor Wanyama, 21. Dennis Odhiambo, 10. Erick Johanna, 7. Ayub Timbe, 11. Francis Kahata, 9. John Avire
Akiba:
John Oyemba, Faruk Shikalo, Joash Onyango, Joseph Okumu, David Owino, Bernard Ochieng, Eric Ouma, Anthony Akumu, Ismael Gonzalez, Ovella Ochieng, Paul Were, Cliffton Miheso, Johanna Omollo, Masud Juma, Christopher Mbamba, Michael Olunga