Aussems ashangaa wabrazili

Tuesday July 16 2019

 

By Thobias Sebastian

KIKOSI cha Simba kimeondoka nchini jana Jumatatu kwenda Afrika Kusini, huku nyota wake wanne wa kigeni akiwamo Francis Kahata na Meddie Kagere wakikwama, lakini Kocha Mkuu, Patrick Aussems akikiri Wabrazili wamemfanyia bonge la sapraizi.

Kagere na Kahata aliyesajiliwa hivi karibuni sambamba na kiungo Msudan, Shiboub Sharaf Eldin na winga Deo Kanda kutoka DR Congo wamezuiwa kupaa na wenzao kutokana na ishu ya viza, japo mchakato ulikuwa unafanyika ili kesho Jumatano wasepe zao Sauzi.

Msafara wa wachezaji 23 Simba ukiongozwa na Aussems uliondoka saa 4 asubuhi kwenda Sauzi kuweka kambi ya wiki mbili kabla ya kurejea nchini Agosti 5 kwa ajili ya kuwahi Tamasha la Simba Day linalofanyika Agosti 8 ya kila mwaka.

Mwanaspoti lililoweka kambi ya muda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JK Nyerere, lilishuhudia nyota hao sambamba na watu wa benchi la ufundi wakiondoka kuelekea Afrika Kusini, huku nyota hao wanne wakikosekana kwenye msafara huo.

Hata hivyo katika dodosa ikafahamika kuwa wachezaji hao wamekosa viza mapema na kwamba huenda wakaipata leo Jumanne na kuwawezeshe kesho Jumatano kupaa kuwafuata wenzao ili kuwahi programu za makocha wao.

Kocha Aussems aliliambia Mwanaspoti mahala ambapo wanakwenda kuweka kambi ni sahihi kama ilivyokuwa nchini Uturuki ambapo walifanya maandalizi ya msimu uliopita na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Aussems alisema anaamini tatizo la kina Kahata na Kagere litashughulikiwa mapema ili wawahi kambi hiyo aliyodai ni sahihi kwa maandalizi yao ili kufanya vizuri kama ilivyokuwa msimu uliopita walipoenda kujichimbia Uturuki.

Advertisement

“Wachezaji wengine wote wapo safarini wakiwa buheri na salama, na nilipata nafasi ya kuzungumza nao wote huku nikiamini nitakwenda kuwaona na kufanya maandalizi mazuri tukiwa kambini,” alisema Aussems.

Nyota wote wa Simba wakati wanaondoka Dar es Salaam walionekana kuwa na furaha huku wakipiga stori wakiwa wanaingia sehemu ya ukaguzi kabla ya kupanda ndege na kuondoka saa 4:00 asubuhi kama safari yao ilivyopangwa.

KUPIGA MECHI TATU

Kocha Aussems alifichua kuwa, kwa wiki mbili watakazokuwa Sauzi Simba inatarajiwa kucheza mechi tatu za kirafiki kujipima nguvu ili kutesti mitambo kabla ya kuja kuuwasha moto Simba Day, msimu mpya wa Ligi Kuu Bara pamoja na michuano ya kimataifa.

Aussems alisema wamepanga kucheza mechi hizo na timu zenye uwezo ili kupima nguvu na ubora wa yale ambayo watakuwa wanayafanyia kazi nchini humo.

“Tumepanga kucheza mechi nne za kirafiki, tatu tutacheza Afrika Kusini tukiwa kambini na moja kwenye Simba Day, japo mpaka sasa haijafahamika majina ya timu, ila ratiba yangu kiufundi ipo hivyo, kabla ya kuanza msimu mpya,” alisema Aussems.

WABRAZILI WAMSAPRAIZI

Aidha Kocha Aussems alisema kama kuna kitu ambacho kimemsapraizi ni usajili wa Wabrazili ambao alisema anataka kutumia kambi ya Afrika Kusini ili kuwaona wachezaji hao watatu kujua ubora na viwango vyao kwa vile anadai hajawahi kuwaona wakicheza.

“Wachezaji hao Wabrazili na wengine wote nitakwenda kuona ubora na ufundi wao tutakapokuwa kambini na katika mechi tutakazocheza zitanisaidia kujua jinsi ya kuwatumia, ila naamini msimu ujao tutakuwa bora zaidi kuliko msimu uliopita,” alisema.

Simba iliwasajili Wilker Henrique Da Silva, Tairone Santos Da Silva na Gerson Fraga Vieira wanaocheza kwenye nafasi ya beki na straika, huku pia ikiwa na Shiboub Sharaf Eldin kutoka Sudan, Deo Kanda na Francis Kahata wanaougana na wageni watatu waliobakishwa msimu uliopita ambao ni Clatous Chama, Kagere na Pascal Wawa.

KAPOMBE NAYE NDANI

Katika msafara ulioondoka, miongoni mwa nyota waliosafiri ni beki aliyekuwa majeruhi kwa muda mrefu, Shomary Kapombe ambaye kwa miezi karibu sita alikuwa nje akijiuguza tangu alipoumia mwaka jana akiwa kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars, iliyokuwa Sauzi.

Kapombe alisema alifanya mazoezi na ratiba ambayo alipangiwa na madaktari wake kwa muda wote ambao alikuwa anaumwa, na amefanya vizuri kiasi amepona na yupo katika hali ya ushindani.

“Naendelea vizuri nipo tayari kwa ushindani na ndio maana nipo katika orodha ya nyota wanaokwenda kambini katika maandalizi ya msimu ambako huko kiasi kikubwa tutakuwa tukifanya mazoezi magumu,” alisema.

“Mashabiki wasiwe na wasiwasi naendelea vizuri na nitafanya kile wanachohitaji kutoka kwangu ili kuifikisha timu katika malengo yake ambao wamejipangia.”

Advertisement