Aussems afunguka jeraha la Nyoni

Wednesday January 9 2019

 

Zanzibar. Kocha wa Simba, Patrick Aussems amesema kukosa huduma ya beki Erasto Nyoni kwa wiki tano ni pigo katika mipango yake ya msimu huu.

Akizungumza na gazeti hili, Aussems, alisema Nyoni atakaa nje ya uwanja wiki tano hadi mwezi ujao na atakosa mechi zote tatu za awali za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba itaanza kucheza mechi ya kwanza Jumamosi ya wiki hii dhidi ya JS Saoura ya Algeria kabla ya kuivaa AS Vita ya DR Congo ugenini.

Simba itatupa karata ya tatu kwa kupepetana na kigogo cha soka Afrika Al Ahly ya Misri kati ya Februari Mosi au Pili, mchezo ambao utachezwa nchini humo. Aussems alisema Nyoni ameumia vibaya baada ya kufanyiwa vipimo zaidi katika Hospitali ya Taifa, Muhimbili, Dar es Salaam.

Hata hivyo, Aussems raia wa Ubelgiji alisema ana kikosi kipana cha wachezaji ambao wataziba pengo ya mchezaji huyo mwenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani.

“Siyo Nyoni pekee aliyepata majeraha ingawa pigo lake ni kubwa kulinganisha na wachezaji wengine ambao maumivu yao ya kawaida na wanaweza kucheza,” alisema Aussems.

Kocha huyo alisema amechukua tahadhari kwa kuwapa mapumziko Meddie Kagere, James Kotei, John Bocco na Emmanuel Okwi.

Advertisement