HISIA ZANGU : Aussems achanganye za Mourinho na Pep akizingatia nidhamu

Tuesday February 12 2019

 

By Edo Kumwembe

SIMBA ikifungwa leo Jumanne imekwisha. Kwahiyo watakaa nyuma na kucheza kwa nidhamu kama Jose Mourinho wa zamani? Au watashambulia na kushinda mechi kama Pep Guardiola wa sasa? Au watachanganya vyote ili kusaka matokeo mazuri?

Maswali mawili yanayoweza kusumbua akili. Simba ikifungwa leo itabakiwa na pointi tatu tu. Al Ahly itakuwa na pointi 10 na kwa asilimia kubwa itakuwa imefuzu. Simba ikishinda leo itafikisha pointi sita na itaweka hai matumaini ya kufuzu.

Inagawanya vipi hisia zao leo? ni swali gumu. Inahitaji nidhamu kubwa katika maeneo yote ya uwanja. Hofu yangu kubwa ni Simba kufungwa. Sababu ni moja tu. Itataka kushinda na itashambulia kwa nguvu zote na kuacha mianya mingi nyuma yao.

Nidhamu ya kujilinda na kushambulia ipo? Sidhani kama ipo katika kiwango kinachotakiwa. Ni kosa ambalo kocha, Patrick Aussems amefanya katika mechi mbili zilizopita dhidi ya AS Vita na Al Ahly. Hasa katika mechi dhidi ya Al Ahly.

Aussems alikwenda ugenini kujaribu kushinda mechi hizi. Jaribu kutazama pambano dhidi ya Al Ahly. Timu ilijifungua katika dakika ya kwanza tu. kulikuwa na ‘one against one’ mara nyingi tu kati ya walinzi na washambuliaji wa Al Ahly.

Hisia hizi zinaanzia katika kujidanganya kwa hali ya juu kati ya kocha na mabosi wake. kwamba wanakwenda ugenini kusaka pointi tatu muhimu. Hawaangalii sana uwezo wa wapinzani wao dhidi yao. Unakwenda kucheza na watu waliofika fainali mbili tofauti msimu uliopita na bado unakwenda kushambulia.

Advertisement

Niidhani kwanza wangeubana uwanja kisha wakawasoma wapinzani wao. Hawakufanya hivyo. Walijaribu kupishana nao kuanzia dakika ya mwanzo tu. matokeo yake kulikuwa na mgawanyiko mkubwa katika eneo la kiungo na eneo la ulinzi. Al ahly ikapita katika shimo hilo hilo.

Leo Aussems anapaswa kuufunga uwanja kwanza na kutoendana na kelele za mashabiki au viongozi wa timu hiyo ambao watataka mashambulizi ya mara kwa mara. Ninachojua ni kwamba Al Ahly itafurahia kushambulia na Simba ili wapate nafasi ya kufanya mashambulizi ya kushtukiza.

Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola ana uwezo mkubwa wa kucheza soka la kushambulia na timu yake isipoteze mpira katika eneo la mwisho. Anajua wakipoteza watampa adui nafasi ya kufanya mashambulizi ya kushtukiza. Lakini hapo hapo Pep ana uwezo mkubwa wa kutengeneza kikosi chenye nidhamu ya kukaba wakati hawana mpira. Simba hawana nidhamu hiyo.

Kocha wa zamani wa Chelsea, Real Madrid, Inter Milan na Manchester United, Jose Mourinho ana uwezo mkubwa wa kuikaba timu pinzani. Sasa hivi makali yake katika kufunga geti yamepungua lakini zamani alikuwa ana uwezo wa kuhitaji sare na akaipata. Aussems akiichezesha Simba kwa staili hii pekee bado haiwezi kuisaidia sana timu katika msimamo wa kundi lake. Wanahitaji matokeo.

Hapa ndipo ambacho Mzungu wa Simba inabidi achanganye mambo yote haya kwa pamoja. Bahati yake kama Simba itatangulia kupata bao lakini kama Al Ahly itangulia kupata bao mechi inaweza kufa moja kwa moja kwa upande wa Simba. Kujilinda zaidi hakutawasaidia kwa sababu watakachofanya Al Ahly ni kumiliki tu mpira katika eneo lao na katikati ya uwanja, kitu ambacho wana uwezo nacho kwa asilimia kubwa.

Eneo jingine ambalo linaipa Simba wakati mgumu ni eneo la mipira ya adhabu kuelekea katika lango lao. Imefungwa mabao matatu ya vichwa katika mechi mbili za Vita na Al Ahly. Hapa naweka kando bao la Walter Bwalya katika pambano dhidi ya Nkana Red Devils.

Hawa akina Paschal Wawa na Juuko Muruhid ni wachezaji wa kulipwa wa kigeni lakini katika eneo hilo hawajaipa Simba msaada mkubwa. Wamecheza mechi nyingi za kimataifa lakini katika eneo hilo hawajaisaidia Simba.

Hii ilikuwa siri iliyojificha kwa muda mrefu kwa sababu ligi yetu ina timu nyingi dhaifu ambazo hazikuonyesha udhaifu huu wa Simba. Mipira mingi ya kona au krosi inapotea bure. Kwa sasa mshambuliaji wa ligi yetu ambaye unaweza kumuogopa kwa mipira ya juu ni Heritier Makambo wa Yanga.

Mechi tatu zilizopita za kimataifa zimefichua tatizo hili la Simba na Waarabu watakuwa wameisoma Simba na ndio maana walipata bao la kuongoza kwa kutumia njia hii pale Alexandria. Wajitahidi kujirekebisha kwa kiasi kikubwa vinginevyo katika mpira wa kisasa mipira ya kona au faulo inakuwa kama penalti tu.

Kila la kheri Simba. Itaingia uwanjani kulipigania taifa lisifedheeke baada ya zile mechi mbili zilizopita ambazo binafsi naamini hazijawafedhehesha Simba, zimeifedhehesha ligi yetu. Simba ni mbabe wa ligi hii na kwa mbali zaidi ni timu iliyosajili vizuri msimu uliopita lakini bado imefungwa mabao 10 katika dakika 180 zilizopita za michuano ya kimataifa.

Advertisement