Aussems: Nitawasaprize Mwadui

Muktasari:

Kocha huyo bado anatafuta kombineshe bora ya safu yake ya ushambuliaji Simba

Shinyanga. Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems huenda akapangua kikosi cha kesho Jumapili kwa lengo la kuhakikisha wanapata ushindi.

Aussems anajaribu kutafuta kila mbinu ili apate matokeo mazuri baada ya kufungwa na Mbao bao 1-0 ikiwemo sare dhidi ya Ndanda.

Mazoezi ya Simba yamefanyika jioni ya leo kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga, tayari kwa mchezo wa kesho dhidi ya Mwadui FC.

Aussems amesema lolote linaweza kutokea katika kikosi hao kesho Jumapili pamoja na kuonekana Emmanuel Okwi ataanzia benchi.

"Maandalizi yapo vizuri na vijana wapo vizuri, ni kweli kuna mabadiliko, lakini mabadiliko hayo hayazuii kuwatumia wachezaji waliopo nje, nina wachezaji wengi hivyo kuonekana kwa Okwi kuwa ataanzia benchi inaweza kuwa ni 'surprise' kesho.

Katika mazoezi ya leo jioni kwenye Uwanja wa Kambarage Mbelgiji huyo ameonekana kumwazisha kinara wa ufungaji Meddie Kagere aliyeanzia benchi mechi iliyopita atashirikiana na Bocco.

Okwi kesho ataanzia benchi huku James Kotei akianza kikosi cha kwanza kuchukua nafasi ya Mohamed Ibrahim.

Aussems amemrudisha Kagere kikosi cha kwanza baada ya mechi iliyopita kumwanzisha Mo kucheza nafasi ya Kagere lakini mpango wake wa kupata mabao haukumsaidia.

Kagere ndiye mchezaji pekee wa Simba aliyeifungia timu hiyo mabao matatu katika mechi mbili walizoshinda.

Wachezaji watakaoanzia benchi katika mchezo wa kesho ni pamoja na Okwi, Salamba, Ndemla, Mo Ibrahim, Rashidi Juma, Kaheza, Gyan, Dida, Bukaba na Abdul Suleiman

Kuhusu uwanja walisema, "Huu uwanja sio rafiki kama ule wa Kirumba hauna ubora ila tutapambana maana lengo letu ni kufanya vizuri, Mwadui ni timu nzuri hatuwezi kuingia kwa kuwadharau."