Aussems: Nilipogoma kupangiwa kikosi shida ikaanza

Saturday December 7 2019

Aussems-Nilipogoma -kupangiwa- kikosi -shida- ikaanza-Simba -KOCHA Patrick Aussems-KUFUKUZWA-SIMBA SC-MRITHI WA AUSSEMS-MWANASPORT-USAJILI-WACHEZAJI-

 

By Khatimu Naheka

KOCHA Patrick Aussems kwa sasa yupo kwao akitafakari kilichomkuta ndani ya Simba baada ya klabu hiyo kumsitishia mkataba wake hivi karibuni.

Siku aliyoondoka alifanya mahojiano mafupi ya dakika 15 na kufunguka mambo kadhaa kabla ya kusepa, jambo lililowafanya mabosi wa Msimbazi kuanza kumjibu kwamba alikuwa kocha wa ovyo tofauti na jina na heshima aliyopewa, wakidai hata kuandika ripoti ilikuwa shida kwake.

Hata hivyo, sasa usichokijua ni kwamba siku mbili baada ya kutimuliwa na Simba, Mwanaspoti ilifanya mahojiano maalum naye kwenye hoteli aliyokuwa akiishi tangu afike nchini na kufunguka mambo mazito kuliko hata aliyoyasema kwenye mahojiano mafupi ya dakika 15 na gazeti hili.

Aussems alifichua ukweli juu ya mambo aliyokutana nayo Msimbazi, maisha yake kwa mwaka mmoja na ushei Simba na hata kufafanua hatua ya kutimuliwa kwake na juu ya ukaribu wake na Mohammed ‘Mo’ Dewji akieleza kwamba bila bilionea huyo, Simba sio lolote si chochote. Kivipi? Mwanaspoti inakuletea mfululizo wa makala ya mahojiano hayo, japo baadhi ya tuhuma tayari zimeshajibiwa na Afisa Habari wa klabu hiyo na aliyewahi kuwa Mtendaji Mkuu, Crescentius Magori na hata Mtendaji wa sasa, Senzo Mazingisa. Endelea nayo...!

ALISHTUKIA MAPEMA

Alipoulizwa amechukuliaje uamuzi wa kufutwa kazi, Aussems alisema; “Ni muda mrefu nilikuwa najua tutafikia hatua hii kati yangu na Simba. Ni muda mrefu walikuwa wanataka kukata shingo yangu, namaanisha kwamba kuna baadhi ya viongozi kila mwezi walikuwa na malengo ya kutaka kuniondoa hapa. Mwezi mpaka mwezi hakukuwa na zuri ninalolifanya katika uso wao, daima walikuwa wakipambana kuhakikisha kazi yangu hapa inaharibika.

Advertisement

“Unajua mimi sio kocha wa kunipangia kipi cha kufanya hasa katika ufundi wa soka, mfano kuniambia mchezaji huyu anatakiwa kucheza au huyu hatakiwi kucheza hii ndio ilikuwa akili yao sasa nilipowakatalia wakatengeneza chuki kwa muda mrefu, hivyo uamuzi huu haukunishtua kabisa kwa kuwa nilikuwa najua kwamba kuna watu wanapambana kunitoa.”

MAISHA YALIKUWAJE SIMBA?

“Maisha yalikuwa mazuri wakati tunaanza hapa na kila kitu kilikwenda sawa. Kidogo maisha yalianza kubadilika baadaye hasa msimu uliopita wakati tukipata mafanikio. Tuwe waungwana, inawezekana Simba ilikuwa inajulikana hata Ulaya, ila kwa kazi ya msimu uliopita iliifanya klabu kujulikana zaidi. Watu walikuwa wanazijua klabu kubwa za Afrika lakini Simba haikuwa na jina kubwa.”

“Tulianza kwa kuhakikisha kwanza tunakuwa na falsafa ya mpira wetu hapa kwa kutafuta wachezaji watakaoendana na falsafa hiyo. Tulifanya kazi kubwa sana msimu uliopita. Wachezaji walikuwa na ubora wa juu kwa mchezaji mmoja mmoja hadi timu nzima. Angalia mchezaji kama Erasto (Nyoni), Kagere (Medie), Okwi (Emmanuel), Chama (Clatous) walifanya kazi kubwa sana, kifupi tulifanya kitu ambacho kilituingiza katika historia kubwa ya klabu hii kwa kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kuchukua taji la ligi hapa Tanzania na Ngao ya Jamii.”

ANGUKO LA SIMBA MSIMU HUU

“Tatizo lilianzia wakati tunaanza kufikiri katika kwenda msimu mpya. Kuna makosa makubwa tuliyafanya. Kuna wachezaji mahiri na bora tuliwaacha. Hapa ndio tulipoanza kuingiza matatizo. Kuna wachezaji waliondoka ambao hadi naondoka hapa sasa sikukubaliana na huu uamuzi wa kuwaacha. Nafikiri uamuzi huu ulitokana na baadhi ya watu. Kuna biashara zao walitaka kuzifanya, walinishinda nguvu wakafanya uamuzi wao wanaoujua.

“Sikukubaliana kabisa na kuondoka kwa wachezaji kama Okwi, Kotei hawa ni wachezaji waliokuwa na nguvu kubwa katika mafanikio ya Simba msimu uliopita. Hata kama kulikuwa na vitu haviko sawa lakini tulipaswa kujaribu kuviangalia na kuvifanyia kazi kama uongozi lakini sio kuwaondoa, kuwaondoa wachezaji kama Kwasi (Asante), Haruna (Niyonzima) au hata Gyan (Nicholas) sikuwa na tatizo lakini hao wawili nilijua uamuzi huu ulifanyika wakati ambao tayari nimeshasaini mkataba mpya. Kama ingekuwa kabla sijasaini nahisi ningekuwa na uamuzi tofauti.

“Unajua katika timu hakuna wachezaji muhimu kama washambuliaji na kila mmoja alikuwa anajua nguvu ya Okwi na morali yake ya ushindani. Alikuwa ni mchezaji ambaye ni mshindani hasa anapovaa jezi ya Simba. Nilijua kwamba tutapata shida na tulipoanza msimu mpya tu washambualiaji wetu tuliotakiwa kuwategemea wawili wakaumia Da Silva akaumia na Bocco akaumia mpaka sasa hawajarudi tunategemea nguvu ya Kagere peke yake na hili likawa ndio msingi wa anguko letu katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kwa kutolewa hatua ya awali.

Vipi kuhusu wachezaji waliosajiliwa

“Kuhusu wachezaji waliosajiliwa wakati tunafikiria wachezaji gani wa kuwaongeza, niliwapa majina ya wachezaji ambao nawahitaji. bahati mbaya zaidi mpaka sasa naondoka kuna mchezaji mmoja tu Kahata ndiye waliyemleta wengine wote hawakuletwa.

Vipi kuhusu usajili wa Wabrazili?

“Usajili wa wachezaji wa Brazili nakumbuka MO alinipigia simu akitaka tushauriane juu ya hawa wachezaji, sikutaka kumdanganya nilimwambia wazi kwamba hiki wanachotaka kufanya ni kama kurusha shilingi wakati unataka kuamua kitu. Upande utakaoangukia hauna namna, unalazimika kukubaliana nao. Unajua Wabrazil hawa hawajui utamaduni wa soka la Afrika. Nilimwambia MO kwamba hii ni kama kamari ngumu.

Walivyokuja mpaka sasa aliwaonaje

“Kila kitu kipo wazi sio lazima mimi Patrick niseme tunaweza kujiuliza wamefanya kazi ambayo tuliitarajia? Nakubaliana na wengi kwamba mchezaji wa kigeni anayekuja hapa ni vyema akawa na ubora mkubwa kuliko mchezaji wa ndani.”

Vipi usajili wake wa Zana Kulibaly

Wakati Aussems akiwataja viongozi wake kuhusika katika usajili mbovu sasa anajibu swali juu ya usajili wa beki Zana Kulibaly ambaye naye aliondoshwa akisema: “Ilikuwa hivi wakati tunaanza msimu uliopita niliona tatizo la beki wa kulia. Wakati huo tulikuwa na Kapombe pekee, nikawaambia viongozi ikatokea Kapombe akiumia au kukosekana kwa namna yoyote tutakuwa na shida tunatakiwa kutafuta beki mbadala wa kulia.

“Nikashauri tunatakiwa kusajili mchezaji mwenye uzoefu mkubwa. Nilipopeleka majina mawili kwa Magori Crescentius alikubalia kila kitu tena alishangilia na kunisifia kwamba nimepata beki mzuri na kuniuliza nimepata wapi beki mzuri kama huyu? Tatizo kubwa la Zana lilikuwa alitumia muda mrefu kuzoea mazingira ya soka la Tanzania, baadaye alianza kubadilika na kuonyesha uwezo mkubwa.

“Shida kubwa ambayo ilikuja kumtokea baadaye ni kitendo cha kuruhusu kusikiliza watu wanasema nini juu yake huwezi kucheza vizuri kila siku, nimecheza mpira pia, alipaswa hata kama watu wanamlaumu asisikilize sana nini watu wanasema badala yake azidi kuongeza juhudi. Hakufanya hayo, presha ikawa kubwa kwake.

Aussems:Bila MO simba haina lolote

Ushindani wa ligi aliuonaje?

“Unajua bado kuna maeneo nayaona kuna changamoto, soka la nchi hii haliwezi kukuwa kama litaendelea kuwa ubingwa unakuwa mali ya Simba, Yanga au Azam zinapocheza timu hizo tatu ndio ushindani mkubwa unaonekana lakini zikicheza na timu zingine matokeo yanakuwa ya kutabirika sana ndio mana timu hizi tatu zikiwa bingwa na kutoka kushindana na mabingwa wengine huko zinapata matokeo mabaya.

“Angalia ligi katika nchi kama Algeria, Misri, Morocco Kongo na hata Afrika Kusini kuna mechi nyingi ngumu katika ligi unaweza kukuta katika ligi kuna mechi mpaka 10 ngumu kila mwisho wa wiki unatarajia kukutana na mechi ngumu. Lakini hapa ni tofauti. Bado kuna timu nyingi nyepesi. Changamoto nyingine kubwa ni viwanja vibovu. Mpira hauwezi kupiga hatua katika viwanja vya namna hii. Nafikiri serikali ya nchi hii inapaswa kuingilia kati katika hili. Kama hawatabadilisha hali ya viwanja kwa haraka nafikiri hata miaka 10 ijayo Tanzania itakuwa na maendeleo yaleyale katika soka, hakutakuwa na tofauti kubwa sana.

Simba kuondolewa Caf ni sababu sahihi kufukuzwa kwake?

“Hatua ya Simba kuondolewa Ligi ya Mabingwa kila mmoja aliumia. Inawezekana ilichukuliwa kama vile wao uongozi ndiyo walioumia peke yao, lakini hata mimi pia iliniharibia, nilikuwa na malengo yangu binafsi pia.

“Nimeona uongozi unasema hiyo ni hatua moja iliyosababisha kunifuta kazi inawezekana ikawa hivyo, lakini nafikiri walipaswa kufanya uamuzi huo wakati uleule tuliotolewa. Kuniacha kuendelea na kazi na kisha kuniongeza mkataba huku tukifanya vizuri katika mechi zetu, kisha uje ufanye uamuzi huo sasa haiingii akilini kabisa naona kama ni ujinga. Unaniondoa sasa wakati timu inaongoza ligi, narudia kuna sababu zao nyingi na huu ulikuwa mpango wa muda mrefu.

Kumbe alimwambia MO kuwa Simba itakuwa na msimu mgumu

“Kuna wakati nilikutana na MO tukiwa tunazungumza nikamwambia kwamba msimu huu tutakuwa na msimu mgumu sana tunapaswa kushikamana sana. Unajua hili linatokana na mafanikio ambayo tuliyapata msimu uliopita. Sasa msimu huu tulitakiwa kuthibitisha ubora wetu na wakati huo kuna watu waharibifu wameshafanya uamuzi wa kuharibu ubora wetu.

“Huu ni mpira kuna lolote linaweza kutokea, angalia labda niulize nani alikuwa anajua mabadiliko ya ratiba ya Caf? Tulipokea taarifa za mabadiliko hayo tukiwa hatua za awali kabisa za maandalizi ya msimu, watu hawaangalii hilo lakini unatakiwa kujiuliza wakati sisi tukiondoa watu wetu muhimu wapinzani wetu nao walifanya makosa kama hayo.

“Simba sio timu kubwa sana kwa mafanikio Afrika angalau sasa naweza kuupongeza uongozi kwa kumalizia uwanja kule Bunju lakini ukiangalia mpaka sasa Simba haina nyumba hakuna uwanja wake wa mazoezi unawezaje kuiita hiyo klabu kubwa Afrika? Tumekuwa tukitumia viwanja vya kukodi kwa muda mrefu mara Boko mara Gymkhana kwahiyo Simba ilipaswa kukua taratibu na katika kukua kuna mambo mengi yanatokea.

Anauonaje uwekezaji wa MO?

“Nimekuwa nikifanya kazi Simba lakini naweza kusema leo Simba imepata mtu sahihi sana, muda si mrefu Simba inakwenda kuwa na viwanja vyake vya mazoezi. Haya ni mafanikio makubwa kwa Simba lakini hii ni hatua iliyowezeshwa na MO, alikuwa kila wakati anaongelea juu ya ndoto zake anazotaka kuona Simba inakuwa klabu kubwa. Amekuwa akifanya makubwa ndani ya timu hii nafikiri bila MO Simba haina kitu chochote katika kupata mafanikio huo ndio ukweli halisi.”

UKARIBU WAKE NA MO DEWJI

“Sidhani kama ni sahihi watu wakisema kwamba niliwadharau viongozi wengine na kumuona MO ndio mtu pekee muhimu. Kuna wakati lazima tuwe wakweli, wakati nafika hapa Simba mara nyingi kila kitu kilikuwa kinamalizwa na MO na yule aliyekuwa Rais aliyeondoka Salim (Abdallah ‘Try Again’) lakini pia kuna dada anaitwa Barbra, mara nyingi hawa ndio watu nilikuwa nakutana nao mara kwa mara katika kufanya majukumu yangu kuwa rahisi.

“Baadaye ndio uongozi ukaja wa bodi, lakini bado nilikuwa naona kila kitu ili kifanikiwe lazima kimalizwe na MO sasa sikuona kama kuna ulazima wa kuanza kutumia njia ndefu tena ya kwenda kumuona mtu mwingine wakati MO yupo. Nafikiri hapo labda ndio kuna baadhi ya watu wakachukia.

Sasa anaiachaje Simba

“Kwasasa mimi sio kocha wa Simba tena, lakini klabu hii itabaki kuwa moyoni mwangu. Hata kama naondoka akili yangu inaniambia kwamba kwa kazi ambayo tumeifanya hapa kuanzia mwanzo wa msimu huu sioni kama Simba inaweza kukosa ubingwa kirahisi na ikitokea hivyo wa kulaumiwa atakuwa kocha mpya atakyekuja badala yangu.

“Ninachoweza kusema ni kwamba nawatakia wachezaji, mashabiki na wanachama kila la kheri katika msimu huu.

“Nitakuwa naifuatilia Simba katika kila mchezo watakaokuwa wanacheza popote nitakapokuwa.”

Anaingaliaje Simba mbele ya Yanga

“ Simba bado ni timu nzuri mbele ya Yanga. Nafahamu kwamba Yanga imekuwa na mabadiliko msimu huu hilo ni kweli lakini bado sidhani kama wanaweza kuitingisha Simba sana katika mbio za ubingwa, nimeona wanapata matokeo lakini sio kwa kiasi kikubwa kuna maeneo wanapata shida kidogo, nafahamu kwamba mwisho wa msimu mbio zitakuwa baina ya timu hizi. Labda wasiwasi wangu ni jinsi gani Simba itaendelea baada ya mabadiliko ya benchi lao la ufundi na hata wachezaji kuwa katika utulivu.

Advertisement